WANGA AOMBA NAMBA YANGA

NA ALLY KAMWE,NAKURU


STRAIKA wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga, amesema yupo tayari kucheza Yanga au timu yoyote ya Tanzania kwa mara nyingine baada ya kuachana na Azam mwaka 2016.

Wanga aliwahi kuichezea Azam, lakini hakuwa na msimu mzuri na kuamua kuachana na timu hiyo ili kuendelea na masomo nchini kwao Kenya.

Kwa kipindi chote baada ya kuachana na matajiri hao wenye maskani yao Chamazi, Dar es Salaam, amefanikiwa kucheza timu za Tusker na sasa Kakamega Homeboyz.

Wanga alifunga mabao mawili kwenye ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Yanga, katika mchezo uliochezwa juzi Uwanja wa Afraha, Nakuru.

Gazeti hili lilimtafuta na kufanya naye mzungumzo, huku akionyesha hamu kubwa ya kutaka kurudi tena Tanzania, akihisi ana deni baada ya kushindwa kutamba na Azam wakati ule.

“Natamani kurudi tena kucheza Tanzania, wakati ule sikufanikiwa kuonyesha kiwango kizuri, lakini hivi sasa kama kuna timu itanihitaji nipo tayari.

“Najua sina historia nzuri na Tanzania, lakini natumai nikipata timu safari hii nitakua na kitu cha kuonyesha, popote nitakapopata nafasi nitacheza,” alisema Wanga.

Hivi sasa timu za Tanzania zipo katika vuguvugu la kusaka wachezaji baada ya ligi hiyo kumalizika hivi karibuni na Simba kutwaa ubingwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*