RONALDO ACHAFUA HALI YA HEWA REAL MADRID

MADRID, Hispania


HUENDA tetesi za Cristiano Ronaldo kuondoka Real Madrid zikashika kasi zaidi, baada ya staa huo kutoonekana kwenye picha za kuzindua jezi mpya za klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

Jezi mpya za nyumbani na ugenini zilitambulishwa rasmi mapema wiki hii na wachezaji wa klabu hiyo, akiwemo nahodha Sergio Ramos, Marcelo, Keylor Navas, Toni Kroos na Isco.

Ronaldo hakuwepo kwenye picha hizo, lakini Gareth Bale ambaye baada ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya alinukuliwa akisema kwamba anatafakari kuhusu hatima yake, alionekana katika utambulisho wa jezi hizo.

Hata hivyo, inakumbukwa misimu miwili iliyopita Ronaldo hakuhusika kwenye zoezi lolote la utambulisho wa jezi za Madrid, sababu kubwa ikiwa ni kuepusha mgogoro wa kibiashara kati ya kampuni ya Nike na Adidas.

Ronaldo anadhaminiwa na Nike ambao alisaini nao mkataba wa maisha, Novemba mwaka 2016, ulioripotiwa kuwa na thamani ya dola bilioni moja, wakati jezi za Madrid zinatengenezwa na kampuni ya Adidas.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*