MWAKYEMBE MGENI RASMI FAINALI KAMBE LA AZAM

NA JACKLINE LAIZER


 

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa fainali wa Kombe la Azam.

Fainali hiyo itawakutanisha Singida United na Mtibwa Sugar, itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini hapa.

Akizungumza mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, alisema Dk. Mwakyembe ndiye atakayekuwa mgeni rasmi wa fainali hiyo.

Kihamia alisema kuhusu maandalizi ya fainali hiyo yameshakamilika kwa asilimia kubwa na kinachosubiriwa ni timu kuingia uwanjani.

Alisema wamefanya maandalizi mazuri kwa kushirikiana na viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA).

“Uwanja upo katika hali nzuri, mimi mwenyewe nikishirikiana na viongozi wa chama cha soka mkoa, tumeukagua, ninawaomba wadau na wapenzi wajitokeze kwa wingi kushuhudia fainali hiyo,” alisema Kihamia.

Kihamia aliwashukuru viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kuupa heshima Mkoa wa Arusha kuandaa fainali hiyo.

“Sisi kama watu wa Arusha kupitia fainali hii tumejifunza jambo la msingi na kubwa sana tuwe na timu yenye ushindani ambayo itafika katika hatua hii.

Tuwe na timu itakayoshiriki Ligi Kuu na kwa kudhamiria hilo tulishaanza mipango na tupo katika hatua za mwisho za kutangaza timu tuliyoichukua ya Ligi Daraja la Kwanza,” alisema Kihamia.

Viingilio vya fainali ya kombe hilo ni Sh 10,000 kwa Jukwaa A, Sh 2,000 kwa Jukwaa B1 na B2 na Sh 1,000 kwa Jukwaa C.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*