WACHEZAJI YANGA WAWEKWA ‘KITIMOTO’

NA ZAINAB IDDY


 

WAKATI kikosi cha Yanga kikitarajiwa kuondoka leo kwenda nchini Kenya kushiriki michuano ya Sportpesa, uongozi wa klabu hiyo jana ulilazimika kuwaweka wachezaji ‘kitimoto’ na kuwaambia mambo mazito baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika.

Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, wameambulia nafasi ya tatu msimu huu nyuma ya Azam FC iliyoshika nafasi ya pili, huku Simba wakitwaa ubingwa.

Licha ya kumaliza nafasi ya tatu, Yanga wamekumbwa na ukata mkubwa hali iliyowafanya baadhi ya wachezaji kuigomea safari ya kwenda nchini Algeria ambako walikwenda kucheza na USM Alger katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Baada ya ligi kumalizika, Yanga sasa inajiandaa kushiriki michuano ya Sportpesa ambayo imewafanya viongozi kuacha shughuli zao na kuwaita wachezaji faragha kuzungumza nao.

Katika mazungumzo hayo, viongozi waliwasisitiza wachezaji kuhusu kujituma ili wajitangaze wenyewe kwani viwango vyao vinaweza kuonekana na kusajiliwa na timu zenye uwezo mkubwa kifedha nje ya nchi.

Taarifa za kutoka ndani ya kikao hicho kizito zinadai kuwa viongozi wamekiri mbele ya wachezaji kuwa hali ya kiuchumi ndani ya klabu hiyo ni mbaya, lakini pia kuwataka kwenda nchini Kenya kwa ajili ya kujitangaza wenyewe.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kikao kilihudhuriwa na wachezaji wote isipokuwa Kelvin Yondani, Andrew Vicent ‘Dante’ na Juma Abdul ambao wametajwa kuwa na udhuru.

“Kikao kilianza saa tatu asubuhi na kumalizika saa sita mchana, viongozi waliokuwepo ni Katibu Mkuu, Charles Mkwasa na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Hussen Nyika, ambao walitupongeza kwa nafasi tuliyoshika licha ya hali ngumu ya kiuchumi iliyopo.

“Lakini pia uongozi umeelezea hali halisi ya kiuchumi iliyopo kuwa hairidhishi, hivyo tuende nchini Kenya kwa lengo la kujitangaza ili tupate nafasi ya kucheza soka la kulipwa.

“Kuhusu suala la malipo ya mshahara na fedha za usajili tunazodai tumetakiwa kusubiri hadi tutakaporejea nchini kwani bado wanafanya mchakato wa kutafuta fedha hizo,” kilieleza chanzo hicho.

Hata hivyo, BINGWA lilimtafuta Mkwasa ambaye pia alikiri kufanya mazungumzo na wachezaji lakini hakutaka kuweka wazi mambo  yaliyozungumzwa.

“Ligi imeisha ni lazima tukae na wachezaji kuelezana tulipofikia kama ilivyo kawaida tunapokutana nao kabla ya mashindano, lakini lengo ni kuzungumzia hali halisi iliyopo ndani ya klabu.

“Sidhani kama ni busara kusema nini tumezungumza, haya ni masuala ya kiofisi yanayotuhusu viongozi na wachezaji tu, lakini ni kweli tumekutana na wachezaji leo (jana) asubuhi,” alisema Mkwasa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*