NYOTA 10 YANGA WAJIPELEKA SIMBA

 HUSSEIN OMAR NA WINFRIDA MTOI


 

BAADA ya tetesi za kiungo wa Yanga, Papy Tshishimbi kutakiwa na Simba, kigogo wa juu wa Wekundu wa Msimbazi hao, amesema zaidi ya wachezaji 10 wa watani wao hao wa jadi wamekuwa wakiwapigia simu kuomba kutua Msimbazi.

Akizungumza na BINGWA jana kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, kigogo huyo wa Simba alisema  Tshishimbi ni miongoni mwa wachezaji walioomba kusajiliwa na timu yao, huku wengine akishindwa kuyataja majina yao.

Alisema wanasikia taarifa nyingi wakihusishwa kutaka kuwasajili baadhi ya wachezaji kutoka Yanga, lakini ukweli ni kwamba, hawana mpango huo kwa  sababu wanasajili kwa kufuata mapendekezo ya mwalimu ila ukweli   nyota hao ndiyo wanaopiga simu.

“Sisi hatujafanya mazungumzo na Tshishimbi, yeye ndiyo amepiga simu kuomba kuja Simba, tena kuna wachezaji wengine wameomba, wanafika 10, hadi inachosha, ila sisi tunasajili kwa matakwa ya mwalimu kama itatokea akahitaji mchezaji huko sawa,” alisema.

Simba tayari wameshakamilisha usajili wa wachezaji wawili ambao ni Marcel Kaheza wa Majimaji na Adam Salamba aliyekuwa Lipuli FC, kila mmoja akisaini mkataba wa miaka miwili.

Lakini wakati kigogo huyo akiyasema hayo, BINGWA lilipomtafuta Tshishimbi alikana kuwa na mpango wa kwenda Simba akiweka wazi shauku yake ya kuendelea kuitumikia Yanga.

Kiungo huyo ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), aliyejiunga na Yanga msimu uliomalizika mapema wiki hii, alisaini mkataba wa miaka miwili tayari akiwa ametumikia mwaka mmoja.

Tshishimbi alisema taarifa hizo za yeye kwenda Simba ni mpya kwa     sababu hajawahi kuzungumza na kiongozi yeyote wa timu hiyo juu ya suala la usajili.

“Mimi sijui lolote, mimi bado nina mkataba na Yanga, hivyo siwezi kufanya lolote kwa sasa,” alisema Tshishimbi.

Katika kuthibitisha hilo na kuwaondoa hofu mashabiki wa Yanga, jana alikuwa miongoni mwa kikosi kilichofanya mazoezi kujiandaa na michuano ya SportPesa Super Cup itakayoanza wikiendi hii nchini Kenya.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini, Dar es Salaam, Tshishimbi alionekana kujifua vilivyo ili aweze kuwa fiti zaidi.

Katika orodha ya majina ya wachezaji wa Yanga wanaosafiri kwenda Kenya leo, Tshishimbi ni miongoni mwao wengine wakiwa ni Youthe Rostand, Ramadhan Kabwili, Thabani Kamusoko, Hassan Kessy, Gadiel Michael na Mwinyi Haji.

Pia, wapo Pius Buswita, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Pato Ngonyani, Ibrahim Ajib, Maka Edward, Yohana Nkomola, Matheo Athony, Amissi Tambwe, Juma Mahadhi, Said Makapu, Said Mussa, Yusuph Mhilu na Rafael Daudi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*