ALI KIBA ASHINDWA KUIBEBA TIMU YAKE RAMADHANI CUP

 

NA MWANDISHI WETU


 

 

MWIMBAJI wa muziki wa Bongo Fleva, Ali Kiba, juzi usiku ameshindwa kuisaidia timu yake ya Binslum & Risa na kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba Oil ya Morogoro.

Timu hizo zilikutana katika michuano ya Ramadhani Cup inayoendelea kwenye Kituo cha JK Park kilichopo Kidongo Chekundu, Kariakoo jijini Dar es Salaam.

Binslum & Risa ndio walikuwa wa kwanza kupachika bao dakika za mwanzo za mchezo huo, baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Kiba.

Kiba alipoteza nafasi mbili za wazi ambazo zingeisaidia timu yake kuongoza kwa zaidi ya mabao 3-0, lakini baadaye Simba Oil walisawazisha dakika chache kabla ya mapumziko.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kipindi cha pili, pamoja na mabadiliko yaliyofanywa pande zote mbili lakini ulimalizika kwa sare hiyo ya 1-1.

Baada ya mchezo huo kumalizika kulitokea mtafaruku baada ya kocha mchezaji wa Binslum & Risa, Nassor Binslum, kudai dakika zilikuwa hazijamalizika.
 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*