PLUIJM AIFUNGIA KAZI MTIBWA SUGAR

NA CLARA ALPHONCE, SINGIDA


 

 

KOCHA wa Singida United, Hans van der Pluijm, ameamua kuwapumzisha baadhi ya nyota wake katika michezo miwili ya Ligi Kuu Tanzania Bara iliyobaki, akihifadhi nguvu kwa ajili ya fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania (Azam Federation Cup) inayotarajia kufanyika Juni 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Katika mchezo huo wa fainali, Singida United itavaana na Mtibwa Sugar ambapo mshindi ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Akizungumza na BINGWA mjini hapa juzi, Meneja wa Singida United, Ibrahim Mohamed, alisema Pluijm amefikia uamuzi huo kwa kuwa hana cha kupoteza katika ligi, hivyo ni bora awekeze nguvu kwenye fainali hiyo muhimu kwao.

“Haruna cha kupoteza kwenye ligi, michezo hiyo miwili haiwezi kutushusha kutokana na nafasi tuliyopo, hivyo kwenye mechi ya Majimaji, viongozi wameamua kuwapa nafasi vijana ambao hawapati nafasi ili kiwapumzisha baadhi ya wachezaji nyota kwa ajili ya fainali,” alisema.

Alisema timu yao ikiwa na kikosi kamili, inatarajia kuondoka Singida Mei 20, mwaka huu kuweka kambi jijini Arusha kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo ya fainali.

Singida United iliyopanda daraja msimu uliopita, imeonyesha upinzani wa hali ya juu katika Ligi Kuu Tanzania Bara kama ilivyokuwa Kombe la Shirikisho Tanzania.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*