UKWELI MIL 600/- ZA YANGA

*CAF yataja siku zitakazotolewa, yasema Yanga wakituliza akili, kuongezwa midola ya kumwaga

NA MICHAEL MAURUS

MARA baada ya Yanga kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa sasa mashabiki wao wamekuwa wakitambia kitita watakachopokea kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kutokana na mafanikio yao hayo.

Wapo waliofika mbali kwa kuzipangia matumizi fedha hizo, wengi wakiamini zitalipa madeni ya mishahara ya wachezaji na kuwawezesha kusajili wachezaji wenye uwezo wa hali ya juu ili kukiimarisha zaidi kikosi chao kuelekea hatua inayofuata.

Lakini pia, wapo viongozi wa Yanga ambao wameanza kufikiria ni vipi wanaweza ‘kuzipiga’ fedha hizo kama ilivyo tamaduni ya baadhi ya mabosi wa soka hapa nchini.

Wengine wamekuwa wakifika mbali zaidi kwa kuanzisha chokochoko ili kuwachafua wale wenye misimamo inayoweza kuwazuia kula fedha hizo.

Kwa upande wa nje ya Yanga, kuna mashabiki wa Simba ambao tayari wamepanga matumizi ya fedha za watani wao hao wa jadi katika kulipa madeni na mwisho wa siku, kubainika Wanajangwani hao hawatabakiwa na hata senti tano.

Lakini wakati hayo yote yakiendelea, BINGWA limebaini wengi hawafahamu kiasi halisi ambacho Yanga watapata na ni muda gani watapewa fedha hizo na CAF.

Kwa mujibu wa mtandao wa CAF, timu zilizotinga hatua ya makundi ya michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho, zina nafasi ya kuondoka na kati ya Dola za Marekani 275,000 (Sh milioni 600) hadi Dola 1,250,000 (Sh bilioni 2.8).

Hata hivyo, Dola 275, 000 ambazo zimekuwa zikitajwa na watu wa Yanga kuwa wamezipata baada ya timu yao kutinga makundi, zinatolewa kwa timu zitakazoshika nafasi ya nne na ya tatu kati ya timu nne za kila kundi miongoni mwa makundi manne.

Iwapo timu itatinga robo fainali, itapata Dola 350,000 (Sh milioni 795.7), huku zitakazofika nusu fainali zitapata Dola 450,000 (Sh bilioni moja), wakati mshindi wa pili ni Dola 625,000 (Sh bilioni 1.4) na mshindi atavuna Dola 1,250,000 (Sh bilioni 2.8).

Kwa maana hiyo, fedha hizo zitatolewa baada ya kuhitimishwa kwa michuano hiyo ambapo ndipo itakapofahamika ni timu gani zilizoshika nafasi mbili za mwisho, yaani ya nne na ya tatu, za robo fainali, nusu fainali, mshindi wa pili na bingwa.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa mchanganuo huo wa fedha hizo za CAF, iwapo Yanga watatuliza akili zao na kujipanga vilivyo kuelekea hatua hiyo inayofuata, wanaweza kuvuna fedha nyingi zaidi ya hizo milioni 600 wanazotambia.

Tayari uongozi wa Yanga umeweka wazi juu ya mpango wao wa kuwagawia wachezaji wao sehemu ya fedha hizo za CAF na nyingine kutumika katika matumizi mengineyo, ikiwamo kulipa madeni.

Kiongozi mmoja wa Yanga alipopewa ufafanuzi huo wa mchanganuo wa fedha watakazopewa na CAF, alisema: “Binafsi nilikuwa nalifahamu hilo, ila nashangaa hata baadhi ya viongozi wenzetu walikuwa wakidhani kuwa tutapewa hizo fedha mara tu baada ya kufuzu makundi.

“Watu wanatakiwa kufahamu kuwa tuna kazi kubwa ya kufanya kusaka fedha za maandalizi ya michuano hii, kwani hizo wanazozitaja tutazipata baadaye na si hivi karibuni,” alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*