MAADILI YASIWE KIGEZO CHA KUTOTATUA MATATIZO HAYA

NA CHRISTOPHER MSEKENA

TUKIWA katika mwezi ambao nyimbo 13 za Bongo Fleva zimefungiwa na mamlaka husika. Ni vyema sasa tukaanza kutafakari mambo muhimu na makubwa kwa ustawi wa sanaa yetu.

Ukiaacha ‘maadili’ ambayo yanapigiwa kelele  na viongozi wenye mamlaka za juu kwenye sekta ya sanaa kuna mambo yenye mashiko na yanayoweza kuacha alama kwenye tasnia ya burudani hayafanyiki na wala hayashughulikiwi kwa nguvu kama vile nyimbo kufungia nyimbo.

Ni aibu kwa miaka minne sasa hakuna tuzo za muziki kwa utetezi kuwa hakuna wadhamini. Kwanini nguvu inayotumika kufuatilia wasanii na kuwafungia nyimbo zao isielekezwe kwenye kusaka wadhamini.

Wasanii wetu wameendelea kushinda tuzo za nje, sisi hatuna za kwetu za kujivunia lakini viongozi wenye mamlaka na sanaa hawazungumzi chochote na wala hawaoni madhara ya kutokuwa na tuzo.

Ubora wa msanii unapimwa kwa tuzo. Mtu anapofanya kazi nzuri na ikaonekana anapaswa kutunukiwa. Je wasimamizi wa sekta hii huwatunukia nini wasanii wanaowasimamia?

Ni vyema tukajitafakari na kuelekeza nguvu za kufungia nyimbo katika kuleta matukio kama ya tuzo ambayo yanaongeza chachu ya ushindani kwenye muziki filamu na sanaa zingine.

Jambo lingine ambao ni vyema likapewa nguvu ni suala la usajili kwa wasanii. Inatia aibu mpaka leo hii mamlaka husika husajili wasanii wake kupitia makaratasi.

Kwanini tusiwekeze nguvu katika teknolojia ili wasanii wengi wanapotaka kujisajili wasajiliwe kupitia mtandao. Mtu anaingia mtandaoni anapakua fomu anaijaza na kuituma kwa barua pepe na cheti chake anatumiwa kwa njia hiyo hiyo.

Kwa sanii kutoka Dar es Salaam ni rahisi kufika kwenye ofisi kusajiliwa lakini vipi wasanii wa vijijini. Vipi wasanii wanaotoka mikoa ya mbali watasajiliwa vipi wakati nauli tu ni kubwa.

Baraza la Sanaa linapaswa kutanua huduma zake za kusajili wasanii. Ni vyema likaelekeza nguvu zake katika mtindo wa kisasa wa dijitali. Msanii aweze kujisajili kupitia simu na vifaa vingine vya Intaneti isiwe lazima kufika ofisini.

Lakini pia hapo hapo kwenye masuala ya kimtandao. Nilikuwa namsikiliza Diamond jana kwenye kipindi The Playlist pale Times FM anasema albamu yake anaiuza kupitia mitandao ya Kenya na ile ya kimataifa ambayo haipo Tanzania.

Tanzania hakuna mtandao ambao unaweza kuuza albamu yake mpaka pale atakapoachia nakala ngumu. Hii ni aibu. Kwanini wasimamizi wa sanaa yetu hawafikirii kutengeneza mazingira mazuri ya wasanii kuuza kazi zao mtandaoni.

Ili msanii anufaike lakini pia serikali iweze kupata kodi yake. Mapato mengi yanapotea lakini hili halionekani.

Suala lingine ni lile la kutokuwa uwanja wa wasanii kufanya matamasha au kumbi kubwa zinazoweza kuingiza mashabiki wengi. Diamond anasema alilazimika kwenda Kenya kwa sababu kule kuna ukumbi unaoweza kwenda sana na maudhui.

Ukumbi ule aliozindulia albamu yake ulikuwa na uwezo wa kwenda sawa na maudhui. Ndiyo maana ulikuwa unabadilika badilika na kufanya sanaa ubunifu uonekane.

Kuna changamoto kubwa kwa wasanii kupata uwanja au sehemu ya kufanyia maonyesho yao kwani katika maonyesho hayo wanawekewa kikomo cha muda wa kumaliza maonyesho yao.

Je wasimamizi wa sanaa hawalioni hili. Kwanini nguvu ya kufungia kazi za wasanii isielekezwe huko kwa wasanii wapate eneo lao nzuri la kutumbuiza ili waweze kulipa kodi na maisha yao yaendelee.

Hayo ni machache ila yapo mengi ambayo ni muhimu yashughulikiwe kwa ustawi wa sanaa yetu. Hatuwezi kukamua ng’ombe ambaye hatumpi malisho.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*