googleAds

KUTOKA VIDEO QUEEN HADI KUINGIA STUDIO, KUIGIZA

 

NA MAREGES NYAMAKA

KUNA msemo wa mitaani usemao ‘hupaswi kuridhika na kazi moja kama chanuo la nywele, kama inatokea mbele yako kuna fursa itumie.’ Msemo huo umeonekana kuwa na maana kubwa sana.

Kama ilivyo katika medani nyingine, kwa siku za hivi karibuni msemo huo unaonekana kuwatokea wengi katika sanaa nchini.

Tumeona jinsi vijana wengi walivyoamua ‘kuchangamkia tenda’ kwa kuhama kutoka upande mmoja na kutua kwingine kujaribu bahati yao na mwisho wa siku, kufanya vizuri.

Orodha ni ndefu, lakini leo BINGWA linakuletea wasanii wachache wanaotesa katika anga ya muziki na filamu ambao awali walikuwa wakifanya shughuli nyingine.

Lulu Diva-Bongo Fleva

Ni mrembo ambaye jina lake lilianza kuwa maarufu kupitia video mbalimbali za wasanii, ikiwamo ya Naogopa ya Mirror kwa sasa akiwa ameonyesha njia nyingine tofauti baada ya kuanza kuimba muziki rasmi.

Mwanadada huyo hadi sasa tayari ametoa nyimbo tatu kali zinazofanya vizuri sokoni ambazo ni Usimuache, Utamu, Give It To Me.

Amber Lulu-Bongo Fleva

Uhodari wake katika video kadhaa huko nyuma hasa kwa upande wa mavazi, ulimfanya kuwa na idadi kubwa ya mashabiki, kitendo kilichomfanya kuingia studio kutoa wimbo.

Miongoni mwa nyimbo alizozitambulisha ni Only You ambayo video yake aliitambulisha Agosti 18, mwaka huu na Watakoma aliyomshirikisha Country Boy.

Giggy Money-Bongo Fleva

Moja kati ya wimbo ambao unafanya vuzuri sokoni hasa katika kumbi za starehe na mitandao ya kijamii hususan kupitia You Tube, ni ya mrembo Giggy Money iitwayo Papa.

Ilikuwa ni video ya wimbo wa Inde wa Dully Sykes aliomshirikisha Harmonize iliyompa umaarufu maradufu Giggy Money kulingana na uwezo mkubwa wa kutimiza majukumu yake kumfanya mtazamaji asiichoke kuitazama.

Kidoa Salum-Bongo Movie

Mashabiki wake walianza kumwona akiwa kama ‘Video Queen’ mbalimbali, ukiwamo wimbo wa Akadumba ulioimbwa na Emmanuel Elibarik ‘Ney wa Mitego’.

Kwa kutambua kuna fursa zaidi ya hiyo, Kidoa akaamua kugeukia upande mwingine ambapo alitua kwenye uigizaji walipo akina Vincent Kigosi ‘Ray’.

Na kwa sasa Kidoa anazidi kuchanja mbuga kwenye Tamthilia ya Huba inayorushwa na kituo cha Dstv kupitia chaneli ya Magic inayotajwa kuwa na watazamaji wengi sana duniani.

Genevieve Mpangala-Bongo Fleva

Jina lake lilitambulishwa rasmi na shindano la urembo pale alipofanikiwa kutwaa taji la Miss Tanzania 2010. Huyu si mwingine bali ni Genevieve Mpangala, akiwa ni mtoto wa aliyekuwa  Meneja wa Klabu ya Yanga, Emmanuel Mpangala.

Genevieve pia aliwahi ‘kuuza sura’ katika video akiwa kama Video Queen wa kazi mbalimbali, ikiwamo ya wimbo Nagharamia wa Christian Bella aliyomshirikisha Ali Kiba.

Kuzungukwa na wasanii hao wenye majina makubwa nchini, kulimshawishi Genevieve kuingia studio na kutoka na wimbo unaokwenda kwa jina la Nana alioutambulisha Aprili mwaka huu.

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*