googleAds

HAPA KIBA, KULE FID Q HAPATOSHI FIESTA MWANZA LEO

NA MWANDISHI WETU

UWANJA wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, unatarajiwa kuwaka moto kesho wakati wasanii wakali wa hapa nchini, wakiongozwa na Ali Kiba, Fid Q, Roma Mkatoliki, Joh Makini, Ben Pol na Nandy, watakapopanda jukwaani kufanya vitu vyao katika tamasha la Tigo Fiesta 2017.

Wasanii wengine ni Jux, Maua, Weusi, Rayvanny, Aslay, Young Killer, Rosa Ree, Lulu Diva, Darasa, Rostam, Bill Nas, Future JNL, Bright, Eduboy na wengineo.

Wakati Kiba akitarajiwa kuiteka Mwanza kwa wimbo wake wa Seduce Me ambao umetokea kubamba vilivyo, Fid Q akiwa katika ‘uwanja wake wa nyumbani’, yaani akiwa kama mkazi wa Mwanza, naye anatarajiwa kupokewa vizuri na wakazi wa jiji hilo.

Ni wazi kuwa, japo Kiba tayari anapewa nafasi kubwa ya kufunika, lakini anaweza kukabiliwa na upinzani wa aina yake kutoka kwa Fid Q, lakini pia wakali wengineo kama Roma, Ben Pol, Joh Makini na hata wasanii wa kike kama Nandy, Maua na wengineo.

Akizungumza na BINGWA jana, Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa Tigo, William Mpinga, alisema kuwa, wakazi wa Mwanza watarajie burudani ya aina yake leo, kwani wasanii watakaopanda jukwaani wamejiandaa vema kufanya mambo makubwa.

Alisema kuwa, tamasha hilo lenye kaulimbiu ya ‘Tumekusomaa’ ambalo ni la 16, linatarajiwa kutua katika miji 15 ambapo hadi sasa, tayari limeshatimua vumbi miji mitatu ambayo ni Arusha, Musoma na Kahama na kwamba baada ya Mwanza, litahamia Tabora, Dodoma, Iringa, Songea, Njombe, Sumbawanga, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara na kuhitimishwa jijini Dar es Salaam.

“Kpitia Tigo Fiesta 2017- Tumekusoma, Tigo imejikita kuinua vipaji vya wasanii wa Kitanzania kama njia mojawapo ya kukuza sanaa nchini. Kama tunavyojua, sanaa imekuwa mojawapo ya nafasi kubwa za ajira kwa vijana wetu na baadhi ya wasanii wetu pia wamepata nafasi ya kupeperusha bendera ya nchi katika nchi za kigeni, kwa hiyo kusaidia kuitangaza nchi yetu. Tuna imani kuwa kupitia ushirikiano huu tutaweza kuwakutanisha wasanii wetu na mashabiki wao, kuwajengea uwezo na hivyo kuwasaidia wasanii wengi zaidi kufikia viwango vya kimataifa,” alisema Mpinga.

Kwa msimu uliopita, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Tigo ilitoa msaada wa madawati zaidi ya 5,700 kwa maeneo yote ambayo tamasha la Fiesta lilifanyika, madawati hayo yaliweza kufanikisha azma ya serikali ya kumuinua mtoto toka kukaa sakafuni hadi dawatini.

“Kwa mwaka huu nguvu nyingi tunazielekeza katika kuhakikisha kwamba mtandao wetu unakuwa na nguvu zaidi za kuweza kuzikabili changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea katika maeneo mengi nchini, hii itatuwezesha sisi kuwa mtandao bora na pendwa kwa Watanzania, bila kujali maeneo waliyopo,” aliongeza Mpinga.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Fiesta, Sebastian Maganga, alisema wakazi wa Mwanza watarajie shoo kabambe na ya aina yake kutoka kwa wasanii wao wakali wa hapa nchini.

“Tutawaletea wasanii wenye hadhi kulingana na mapendekezo ya mashabiki husika wa mkoa huo, tena wale waliojizolea sifa ndani na nje ya nchi,” anasema Maganga.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*