HAWASHIKIKI.. PSG WAMEJIPANGA AISEE, MBAPPE NAYE AMFUATA NEYMAR

 

PARIS, Ufaransa

TAARIFA ya jana ya mtandao wa Daily Mirror, imesema kinda wa Monaco, Kylian Mbappe, amefuzu vipimo kukamilisha usajili wake wa kujiunga na PSG kwa mkopo.

PSG wanamchukua Mfaransa huyo kwa mkopo ili kukwepa rungu la Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), ambalo linahimiza nidhamu ya utumizi wa fedha.

Tayari klabu hiyo imeshamnunua Neymar kwa pauni milioni 200, hivyo kutoa pauni milioni 166 kumsajili Mbappe itakuwa ni kukiuka sheria hiyo.

Ujio wa Mbappe utaiimarisha zaidi safu ya ushambuliaji ya PSG, ambapo sasa kocha Unai Emery atakuwa na Neymar, Edinson Cavani, Angel Di Maria, Julian Draxler, Goncalo Guedes na Lucas Moura.

Kituo cha Runinga cha TF1 cha Ufaransa kimenyetisha kwamba, Mbappe alikuwa kwenye zoezi la kufanyiwa vipimo katika eneo la Clairefontaine, ambako ndiko kikosi cha timu yake ya Taifa ya Ufaransa kinakofanya mazoezi.

Mbappe atakuwa mchezaji wa pili kununuliwa kwa fedha nyingi PSG baada ya Neymar ambaye usajili wake ulitikisa vichwa vya habari barani Ulaya.

Ili kuikwepa Fifa, PSG hawataipa Monaco kiasi hicho cha pauni milioni 166 hadi wakati wa majira ya kiangazi.

Taarifa za PSG kumfanyia vipimo Mbappe ni mbaya kwa klabu vigogo za Manchester City, Real Madrid na Barcelona, ambazo zimekuwa zikimfukuzia nyota huyo kwa muda mrefu.

Mpango wa PSG kumchukua kwa mkopo Mbappe kabla ya kumnunua moja kwa moja, waliwahi kuufanya pia kwa Serge Aurier waliyemtoa Toulouse mwaka 2014.

Kiungo wa PSG, Adrien Rabiot, alisema juzi kwamba Mfaransa mwenzake huyo amemwambia wataungana kwenye kikosi hicho hivi karibuni.

Wawili hao wako pamoja kwenye kikosi cha Ufaransa kinachojiandaa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia za mwakani nchini Urusi dhidi ya Uholanzi na Luxembourg.

“Ndiyo, aliniambia usajili wake kuja PSG ungekamilika Jumanne,” alisema Rabiot mwenye umri wa miaka 22.

“Bila shaka ni habari njema kwa klabu, Kylian ni mchezaji chipukizi ambaye tayari ameshakomaa, akiwa tayari kuwa sehemu ya timu, ni faida kubwa na anatokea Paris,” alisema Rabiot.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*