ZIDANE AMKINGIA KIFUA BENZEMA

MADRID, Hispania

KOCHA Zinedine Zidane, amemkingia kifua staa wake, Karim Benzema, baada yakusema kuwa hawezi kumlaumu kwa kukosa nafasi nyingi katika mchezo ambao Real Madrid waliambulia sare ya mabao  2-2 dhidi ya  Valencia na huku akiyapongeza mabao mawili yaliyofungwa na nyota wake mwingine,  Marco Asensio.

Katika mchezo huo wa La Liga, Asensio aliweza kuziona nyavu mara mbili likiwamo bao alilofunga kwa mpira wa adhabu dakika ya 83 na kuwafanya mabingwa hao watetezi kuambulia pointi wakiwa kwenye uwanja wao wa Santiago Bernabeu.

Pamoja na kuambulia pointi, lakini Benzema alipoteza nafasi nyingi ambazo zingewapa ushindi ikiwamo aliyoipata baada ya  Asensio kusawazisha, lakini mpira aliojitwisha kwa kichwa ukaishia kugonga mwamba.

Hata hivyo, akizungumza mbele ya waandishi wa habari mara baada ya mtanange huo, Zidane ambaye kwa ujumla alionekana kupagawa baada ya Benzema kupoteza nafasi hizo alisema: “Mashabiki wanaweza kufanya chochote kile wanachokitaka. Lakini jambo la muhimu  Karim alipata nafasi na amefanya kazi.

“Usiku wa leo (jana) hakuweza kufunga, lakini hilo si tatizo. Tumebaki tukitabasamu kwa sababu hili ni soka,” alisema kocha huyo.

Alisema kwamba, wakati mwingine mambo huwa yanagoma kwenda, lakini unapaswa kuwa mvumilivu na akasema kuwa hawawezi kukerwa na kile ambacho mashabiki wanakifikiria.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*