googleAds

JEZI ZINAVYOTAJIRISHA VIGOGO EPL

LONDON, England

MBALI na vyanzo vingine vya mapato, klabu za Ligi Kuu England zimekuwa zikiingiza mpunga mrefu kutokana na dili za matangazo. Hebu cheki zinavyofunikana katika mikwanja ya udhamini wa jezi.

Arsenal

Wakiwa na udhamini wa Shirika la Ndege la Fly Emirates, Arsenal wanashika nafasi ya tano kwa kuwa na udhamini mnono wa jezi Ligi Kuu England. Klabu hiyo huingiza pauni milioni 30 kwa mwaka.

Chelsea

Klabu hiyo yenye maskani yake Magharibi mwa Jiji la London, ina udhamini wa jezi kutoka kwa kampuni ya matairi ya magari ya Yokohama.  Kwa kila msimu, viongozi wa Blues huchota pauni milioni 40 kutoka kwa kampuni hiyo ya Japan.

Chelsea wataendelea kuvuna kiasi hicho cha fedha hadi mkataba wao utakapomalizika mwaka 2020.

Everton

Kampuni ya mchezo wa kubashiri ya SportPesa ndiyo wadhamini wa jezi za Everton na kwa makubaliano ya pande mbili klabu hiyo huvuna pauni milioni 9.6 kwa kila msimu. Mkataba wa SportPesa na Everton ya mjini Merseyside utafikia tamati mwaka 2022.

Leicester City

Kampuni ya King Power imekuwa na uhusiano mzuri wa kibiashara na Leicester City. Wadhamini hao hulipa pauni milioni 4 kwa kila msimu. Mbali na jezi, pia uwanja wa nyumbani wa Leicester umepewa jina la King Power.

Liverpool

Wadhamini wakuu wa jezi za Liver ni Standard Chartered na pande mbili hizo zimekuwa zikifanya kazi tangu mwaka 2010. Benki hiyo imekuwa ikiipa Liver kiasi cha pauni milioni 30 kwa msimu. Biashaha hiyo itaendelea hadi mwaka 2022.

Mbali na Standard Chartered, pia jezi za Liver zitakuwa na nembo ya Benki ya Western Union, ambapo kwa dili hilo timu hiyo itakuwa ikivuna pauni milioni 5 mpaka mwaka 2022.

Manchester City

Shirika la Ndege la Etihad litaendelea kuwa wadhamini wa Man City kwa msimu huu na klabu hiyo itakuwa ikivuna pauni milioni 35 kwa kila msimu, hadi pale mkataba wao utakapomalizika mwaka 2021.

Lakini pia, kampuni ya utengenezaji wa matairi ya magari kutoka Korea Kusini, Nexen Tire,  itakuwa ikisaidiana na Etihad kuitajirisha Man City kwani imesaini mkataba wa kuipa pauni milioni saba ili jina lake kutokea kwenye jezi za timu hiyo.

Manchester United

Man United ndiyo klabu pekee yenye udhamini mnono Ligi Kuu England ikiwa inaingiza kitita cha pauni milioni 47 kutoka kwa kampuni ya utengenezaji magari ya Chevrolet.  Man United wataendelea kukinga mkwanja huo hadi pale mkataba utakapokwisha mwaka 2021.

Tottenham

Kampuni ya Bima ya Marekani (AIA) ndiyo wadhamini wakuu wa jezi za timu hiyo na huwa inalipa kiasi cha pauni milioni 35.  Mkataba wa sasa kati ya pande hizo mbili utafikia tamati mwaka 2022.

West Ham

Klabu hiyo imeanza msimu huu wa 2017-18 ikiwa na wadhamini wao wa Bentway. Kampuni hiyo maarufu nchini England kwa michezo ya kamari, huipa West Ham pauni milioni 10 kwa kuitangaza nembo yao kupitia jezi. West Ham hupewa fedha hizo kila baada ya msimu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*