googleAds

PSG WAMFUNGIA KAZI MBAPPE

 PARIS, Ufaransa

TAARIFA zimedai kuwa, PSG wameendeleza jeuri yao ya fedha kwa kuifuata Monaco, wakimtaka Kylian Mbappe, ambaye tangu kufunguliwa kwa dirisha la usajili la majira ya kiangazi amekuwa akiitoa udenda Real Madrid.

Imeelezwa kuwa, klabu hiyo tajiri ya Ligue 1, ambayo hivi karibuni ilitumia kitita cha Pauni milioni 196 kumng’oa Neymar katika kikosi cha Barcelona, inamtaka Mbappe, mwenye umri wa miaka 18.

Jina la straika huyo chipukizi liko mezani mwa mabosi wa PSG na ndiye anayefuata katika orodha ya wachezaji wanaotakiwa kuichezea Ufaransa msimu ujao.

Taarifa zimenyetisha kuwa, tayari PSG wameshakubaliana masilahi binafsi na mchezaji huyo, hivyo kilichobaki ni kuisikiliza klabu yake ya Monaco inataka kiasi gani cha fedha kumwachia.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, huenda PSG wakatoa kitita cha Pauni milioni 180 na kumfanya Mbappe kuwa mchezaji anayeshika nafasi ya pili kwa kununuliwa kwa fedha nyingi duniani, baada ya Neymar.

Mbappe ameshawaambia mabosi wake wa  Monaco kuwa anataka kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi na imeelezwa kuwa, ni kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike ndiyo itakayosimamia mpango huo wa kwenda PSG.

Inafahamika kuwa, mshambuliaji huyo anadhaminiwa na Nike na kampuni hiyo ina uhusiano mzuri na PSG, kwani ndiyo inayosambaza vifaa vyake.

PSG ina mastaa kibao wanaofanya kazi na Nike, na miongoni mwao ni Edison Cavani, Marco Veratti na Neymar, aliyetua mjini Paris hivi karibuni.

Huenda Mbappe havutiwi tena na mazingira ya Monaco, hasa baada ya kuondoka kwa maswahiba zake, Bernardo Silva, Benjamin Mendy waliotimkia Manchester City na Tiemoue Bakayoko aliyetua Chelsea.

Kuna kipindi PSG walimtaka pia beki wa kulia wa timu hiyo, lakini dili hilo lilikwama.

Monaco wanatarajiwa kuwa kwenye wakati mgumu katika safari yao ya kuutetea ubingwa wa msimu uliopita, kwani hata kiungo wao, Thomas Lemar, amekuwa akifukuziwa na Arsenal.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*