googleAds

Upendo kushinda ufahamu

Ilipoishia jana

Roika hakuamini kama anakwenda kukatana uso kwa uso na Ramona, mwanamke ampendaye. Alijiuliza itakuwaje endapo Ramona atajua kuwa yeye alikuwa akimfuatilia.

 Alimuomba Mungu wake mara kumi amuepushe na jambo hilo.

SASA ENDELEA

Lakini dalili za Mungu kumsaidia hazikuonekana mapema, ndiyo kwanza alikuwa chini ya ulinzi mkali, huku akipelekwa kule mkutano ulikokuwa ukifanyika. Alihema juu juu kama mtu anayekwenda kuishiwa pumzi.

Watu wale walimpeleka Roika hadi chumba fulani na kumpigisha magoti. Watu watano wenye bunduki walimzunguka. Mmoja wao ambaye ni mkubwa kati ya wale waliokuwa wamemuweka chini ya ulinzi, alitoka na kuelekea chumba cha mkutano. Alipofika, alimfuata anayeongoza mkutano, ambapo alimsogelea na kumtonya kwa sauti ya chini.

Aliyekuwa akiongoza mkutano huo alishtuka kusikia jambo hilo. Watu wote mle ndani nao walipatwa na wasiwasi baada ya kuona kiongozi wao amebadilika sura kidogo.

“Samahani ndugu wajumbe,” aliongea kiongozi huyo na kutoka pale mezani. Aliongozana na yule mtu aliyekuja kumdokeza jambo, wakaelekea kwenye chumba alichokuwa ameshikiliwa Roika.

Walipofika ndani mtu aliyepeleka taarifa alimwambia mkubwa wake.

“Tumemkamata mtu huyu akiwa anatoka chumba cha mafaili. Na inaonyesha aliingia darini kuja kusikia maongezi ya mkutano.”

“Eti nini?” kiongozi wa mkutano alishtuka.

“Hatujui anakotoka. Tunafikiri ni mpelelezi kutoka idara ya polisi.”

“Mbona ni mtu mweusi na anaonekana si raia wa nchi hii?” kiongozi wao aliuliza.

“Labda ni Mmarekani?” mtu mmoja aliitikia.

“Inawezekana. Mmemuhoji maswali?”

“Tumemuuliza maswali machache. Hajatujibu chochote.”

Kiongozi yule alimsogelea Roika, akamtazama kwa dakika mbili za ukimya na kisha akamuuliza.

“Tuambie wewe ni nani, na umefuata nini hapa?”

Roika alimtazama yule mtu kwa dakika moja na kumjibu.

“Naitwa Fenda namtafuta mdogo wangu aitwae James.”

“Unamtafuta mdogo wako, uliambiwa kuwa anapatikana humu, na umepajuaje hapa?”

“Mimi na mdogo wangu tunafanya biashara ya dawa za kulevya. Kuna watu walimkamata wakihitaji niwape kilo hamsini za mzigo ili wamuachie. Nikaanza kupeleleza maeneo yote ya biashara, ili nimkomboe mdogo wangu.”

Roika alipoongea hivyo, wote mle ndani walitazamana. Waliangaliana wenyewe kwa wenyewe kwa muda wa dakika moja na kisha wakamgeukia tena Roika.

“Watu waliomshikilia mdogo wako unawafahamu?” kiongozi wao aliuliza.

“Hapana siwafahamu,” alijibu Roika kwa kujikaza asionyeshe shaka yoyote japo alikuwa amewadanya.

Watu wawili walitoka ndani ya chumba kile ambapo walielekea nje kuongea machache. Baadaye yule kiongozi wa mkutano alirudi kwenye chumba cha mkutano na kuwaambia wajumbe kuhusu kukamatwa kwa mtu ndani ya himaya yao. Wote mle ndani walishangazwa na taarifa hiyo, akiwemo mrembo Ramona.

“Anadai kuwa, kuna mdogo wake amekamatwa na wafanyabiashara. Hatujui kama anazungumza kweli. Sasa lengo la kuwataarifu ni kutaka kujua je kuna wajumbe ambao wanamshikilia mtu kwa ajili ya kupata mzigo?”

Watu wote mle ndani waligeukiana na baadaye wakamgeukia tena kiongozi wao. Ukimya ulitawala ikionyesha hakuna mtu anayelijua suala hilo. Mmoja wao alionyosha kidole na kuongea jambo.

“Tunaomba  mtu huyo aletwe mbele ya mkutano tumfahamu. Inawezakana ni mpelelezi tu na si kama alivyowaambia,” aliongea mwanamke mmoja aliyekuwa amevaa baibui na nikabu.

Wote mle ndani walimuunga mkono kwa kutikisa kichwa.

Kiongozi huyo aliagiza Roika aletwe mbele ya mkutano.

Roika akiwa chini ya ulinzi mkali, huzuni na hofu vilikuwa vimemtawala. Aliogopa sana kupelekwa mbele ya mkutano,  akihofia kukutana uso kwa uso na Ramona. Mbaya zaidi alikuwa amewadanya watu hao juu ya ujio wake mle ndani. Alijiuliza swali itakuwaje wakijua kuwa yeye ni mfanyakazi wa UN. Maana kitambulisho chake kilikuwa kwenye waleti. waleti yake iliyokuwa mikononi mwao.  Suala la wao kujua kuwa alikuwa amekuja kumfuata Ramona, hakuliwazia sana kwa sababu alijua Ramona hawezi kuwaambia.

Akiwa ampepiga magoti, alishangaa kuona wanamnyanyua na kuanza kupiga nae hatua kuelekea chumba cha mkutano. Sasa alijiandaa kwa lolote.

Roika aliletwa mbele ya mkutano na kupigishwa magoti. Watu wote waligeuka kumtazama. Viongozi wa kikundi cha kigaidi cha Swaba nao walikuwepo.

Roika akiwa mbele yao, aliinamisha kichwa chini asitake kuwatazama ili Ramona asimuone. Ramona naye alimtazama mtu aliyeletwa, asijue ni mpenzi wake. Mmoja wa wapiganaji wa kikundi cha Swaba alimfuta Roika na kumuinua kichwa kwa nguvu.

Ramona alishtuka, alibaki ameduwaa asiyaamini macho yake mawili.

Nini kitafuatia usikose Jumatatu

 


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*