Zahera aweka rekodi ya karne

HUSSEIN OMAR

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ameweka rekodi ya aina yake kwa timu hiyo kushuka dimbani leo kuvaana na Ruvu Shooting bila ya kufanya mazoezi kwa siku mbili mfululizo kutokana na mvua kubwa zinazonyesha jijini Dar es Salaam.

Yanga na Ruvu Shooting zitavaana katika mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, huku Zahera akipania kuibuka na ushindi.

Akizungumza na BINGWA kuelekea katika mchezo huo, Zahera alisema ni mechi ya kufa au kupona kwani amepania kushinda ili kumaliza ligi kwa heshima.

“Tumetoka kufungwa mchezo wetu uliopita, hivyo mchezo wa leo tunapaswa kusawazisha makosa na kufanya vema katika uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.

Alisema kamwe hawatafanya makosa kwenye uwanja wao wa nyumbani kwani wamerekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye michezo iliyopita.

“Tumetoka kufungwa mchezo wetu uliopita, hivyo mchezo wa leo tunapaswa kusawazisha makosa na kufanya vema katika uwanja wetu wa nyumbani,” alisema.

Kwa upande wake, Mratibu wa timu hiyo, Hafidhi Saleh, akielezea sababu ya timu kutofanya mazoezi ni mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam.

“Tulikuwa tufanye mazoezi ya mwisho jana jioni tumeshindwa kwa sababu uwanja umeharibika na juzi vijana walipewa mapumziko ya siku moja kutokana na uchovu wa safari kutoka Musoma tulipocheza na Biashara United,” alisema.

Alisema yote kwa yote wamejipanga kushinda kwani hata Ibrahim Ajib amerejea huku tukimkosa Andrew Vincent ‘Dante’ anayetumikia kadi tatu za njano.

Naye Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Abdulmutik Haji, alisema amekiandaa vizuri kikosi chake ili kupambana na Yanga.

Haji alisema anafahamu ubora wa Yanga  kwa sasa lakini hata yeye ana kikosi kizuri kutokana na matokeo aliyoyapata hivi karibuni.

“Yanga wana wachezaji wazuri na sisi pia tuna kikosi bora, nashukuru wachezaji wote wapo katika hali nzuri, nina matumaini ya kuchukua pointi katika mchezo huo,” alisema kocha huyo.

Alitamba kuwa timu aliyokuwa nayo si kama ilivyokutana na Yanga katika mzunguko wa kwanza kutokana na usajili aliofanya dirisha dogo.

Ruvu Shooting wanatambia safu yao ya ushambuliaji yenye mawinga Emmanuel Martin, Patrick William na mastraika Issa Kanduru, Full Maganga na Said Dilunga aliyefunga mabao 10 hadi sasa.

Yanga kwa sasa wapo nafasi ya pili wakikusanya pointi 80 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakizidiwa na vinara wa Simba wenye pointi 82.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*