Zahera aipotezea Azam

ZAITUN KIBWANA

PAMOJA na Yanga kukabiliwa na mchezo mgumu wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, lakini kocha wa Wanajangwani hao, Mwinyi Zahera, ameonyesha kuwapotezea wapinzani wao kwa kuwaruhusu wachezaji wapumzike kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka badala ya kuendelea na maandalizi ya mchezo huo.

Yanga na Azam zinatarajiwa kuvaana Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa  Taifa, jijini Dar es Salaam ikiwa ni mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana msimu huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, amesema Zahera ametoa mapumziko kwa ajili ya Sikukuu ya Pasaka.

Alisema awali kikosi hicho kilipewa mapumziko ya siku mbili, lakini Zahera ametaka wamalize sikukuu kwanza kabla ya kurejea kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Azam.

Hafidhi alisema kikosi hicho kitakaporejea mazoezini hakitakuwa na mzaha kutokana na ugumu wa mechi hiyo, huku wakiwa na lengo la kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ambapo kwa sasa wana pointi 73 baada ya kucheza mechi 31, huku Azam wakiwa wa pili baada ya kukusanya alama 63 katika mechi zao 31.

“Leo tulipaswa kuendelea na mazoezi lakini hatukufanya hadi Jumanne sikukuu zipite baada ya Zahera kuongeza siku za mapumziko kutoka mbili hadi tatu na baada ya hapo tutaendelea kama kawaida,” alisema Hafidh.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*