‘Yes we can’


NA AYOUB HINJO

LEO ndiyo siku waliyokuwa wakiisubiri Simba kuonyesha ubabe wao dhidi ya timu za Kiarabu zinapokanyaga ardhi ya Tanzania.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, leo watashuka dimbani kucheza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 15 kupita bila kutinga hatua hiyo.

Simba watakuwa wenyeji wa JS Saoura kwenye mchezo utakaopigwa leo saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Tayari kocha wa Simba, Patrick Aussems kutoka Ubelgiji, ameweka wazi kwa uongozi wa klabu hiyo kwamba atahakikisha wanachukua pointi zote tatu.

Kocha huyo anaamini wachezaji wake wana uwezo wa kuandika historia leo kwa kupata ushindi wa kwanza katika Kundi D, lenye timu za Al Ahly ya Misri na AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Aussems alisisitiza wachezaji wake kutumia vizuri kila nafasi ambazo zitatengenezwa uwanjani, sababu hata wapinzani wao wana uwezo mkubwa.

Katika mazoezi ya mwisho ya Simba hapo jana yaliyofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, alikuwa akiongea na washambuliaji wake na viungo mara kwa mara.

Lakini aliwataka mashabiki kuingia kwa wingi kama ilivyokuwa dhidi ya Nkana FC ambao Simba walishinda mabao 3-1 na kujihakikishia kukata tiketi ya kuingia kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu walipofanya hivyo mwaka 2003.

“Tunajua umuhimu wa mchezo wa kesho (leo), lengo letu kushinda michezo yote mitatu ya hapa nyumbani, kuanzia huu dhidi ya JS Saoura.

“Lazima tushambulie ili tupate nafasi za kufunga mabao, ukizingatia wachezaji wetu wana uwezo huo kama ilivyokuwa dhidi ya Mbabane Swallows na Nkana FC,” alisema kocha huyo.

Naye mshambuliaji wa JS Saoura, raia wa Tanzania, Thomas Ulimwengu, ametamba kuwa timu yake itawafunga midomo Simba kwa kuondoka na pointi tatu katika mchezo wa leo.

Ulimwengu anaamini JS Saoura ni timu bora ambayo inaweza kushindana na klabu yoyote kubwa ya Afrika.

“Mchezo wa leo ni muhimu sana kwetu, japo tunajua utakuwa mgumu kutokana na Simba kuwa timu bora hapa Tanzania, yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa.

“Tumejipanga vizuri kuhakikisha tutaondoka na pointi tatu hapa, kikosi chetu kipo vizuri hivi sasa, tunaweza kushinda na klabu yoyote,” alisema nyota huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Simba walianza safari ya kusaka makundi kwa kuwanyuka Mbabane Swallows ya Swaziland jumla ya mabao 8-1, kisha kuhamishia kipigo cha mabao 4-3 kwa Nkana FC ya Zambia.

Nao JS Saoura walianza kwa jumla ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya SC Gagnoa ya Ivory Coast, huku wakiichapa Ittihad Tanger ya Morocco jumla ya mabao 2-1.

Mchezo huo utaongozwa na waamuzi kutoka nchini Botswana, mwamuzi wa kati akiwa ni Joshua Bondo, huku wasaidizi wake wakiwa akina Godisamang Oamogetse na Maomedi Monakwane.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crecentius Magori, akizungumzia mchezo huo, amesema wamezungumza na kocha wao na amewahakikishia ushindi.

“Kocha ametuambia hili ni kundi zuri, tunaweza kushinda mechi zote za Dar es Salaam,” amesema Magori akihojiwa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*