YANGA YAVUNJA UKIMYA

ZAITUNI KIBWANA NA HUSSEIN OMAR

KLABU ya Yanga imevunja ukimya na kusisitiza kuwa kwa sasa hawatajali mechi zilizobaki za watani wao wa jadi, Simba za Ligi Kuu Tanzania Bara na badala yake, wameweka nguvu zao kuijenga upya timu yao kwa ajili ya msimu ujao.

Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku moja baada ya kudaiwa kuwa Yanga imepanga kupiga hodi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba wapinzani wao hao wamalize viporo vyao kisha wao ndio wacheze ili kwenda nao sambamba.

Akizungumza na BINGWA jana, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema akili yao ipo kwenye kutengeneza timu kabambe ya ushindani itakayokuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao, kuanzia katika michuano ya ndani hadi ya kimataifa.

Alisema wapo tayari kucheza mechi zao zote zilizobaki za ligi bila kujali kama Simba wamecheza au la, akisisitiza hata kama wao watamaliza ligi huku watani wao hao wakiwa na mechi 10 mkononi, hakuna shida.

Alisema kwa kuanzia, wanatarajia watakuwa na kikao maalumu na Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera wiki ijayo ili kupata mapendekezo yake juu ya mchezaji wao gani asajiliwe na nani aachwe, lakini pia wale anaotaka watue Jangwani kutoka klabu yoyote ile barani Afrika.

“Tulivyopewa uongozi timu ilikuwa inaongoza ligi, hivyo tumeweka mikakati kushinda mechi zote nne zilizosalia na kujua hatima yetu huko mbele,” alisema.

Mwakalebela alisema kwamba kuthibitisha hawatanii, wameandaa harambee maalumu kwa ajili ya kukusanya fedha zitakazotumika kwa ajili ya usajili.

“Tumeandaa harambee maalumu itakayofanyika Jumamosi hii kwenye ukumbi wa Serena, lengo ni kukusanya fedha za usajili tu kwa ajili ya msimu ujao.

“Kwenye harambee hiyo, tutawaalika wabunge, mashirika mbalimbali ya Serikali na binafsi, taasisi za dini na wadau wote wenye mapenzi ya Yanga kwa ajili ya kukusanya fedha.

“Fedha zitakazopatikana zote zitafanya usajili, tuna imani kwa wageni tutakaowaalika, lengo letu litatimia na Yanga msimu ujao hatutakuwa wa kutufikia,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*