Yanga yatua Moro na hesabu kali

HUSSEIN OMAR NA ZAITUNI KIBWANA

KIKOSI cha Yanga tayari kimetua mjini Morogoro kikiwa na hesabu kali za kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Yanga ndio vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kukusanya pointi 74, wakicheza mechi 31, ambapo wameshinda 23, sare tano na kufungwa tatu.

Akizungumza na BINGWA kuhusiana na maandalizi ya mtanange huo, Kaimu Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Lucas Mashauri, alisema mikakati yao ya sasa ni mizito lakini itabaki kuwa ni siri.

“Tuna mikakati mingi lakini kwanza tutaanza na Mtibwa Sugar tukicheza ugenini, baada ya hapo tutaendelea na mipango yetu kimya kimya, ila kubwa tunataka kumaliza Ligi Kuu kwa kishindo,” alisema Mashauri.

Wakati bosi huyo akiyasema hayo, jana timu hiyo iliyateka baadhi ya maeneo ya vijiji ilipokuwa ikielekea mkoani Morogoro kwa maandalizi ya kuvaana na Mtibwa Sugar ambao walikubali kipigo cha mabao 2-0 katika duru ya kwanza.

Kikosi cha Yanga kinachofundishwa na kocha Mkongomani, Mwinyi Zahera, kiliondoka jana jijini Dar es Salaam kikiwa na wachezaji 20, huku kikibeba matumaini kibao ya kuvuna pointi tatu muhimu.

Wakiwa safarini Yanga walilakiwa na mashabiki wao wakati walipokuwa wakipita barabarani kuelekea mkoani Morogoro, huku wakiwa na shauku ya kutaka kuwaona baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho.

Hata hivyo, Zahera na kikosi chake wameondoka wakiwa na matumaini ya kuibuka na ushindi kutokana na maandalizi kabambe waliyoyafanya kabla ya kuwafuata wapinzani wao hao.

Akizungumzia maandalizi yao, Zahera alisema amekiandaa kikosi chake kwa kiwango cha uhakika ili kuhakikisha wanarejea jijini Dar es Salaam na pointi tatu muhimu zitakazowafanya waendelee kushika usukani wa ligi hiyo.

Aidha, alitamba kuwa kwa kiasi kikubwa ametengeneza kikosi bora ambacho kitaleta ushindani na kupata mafanikio wakianzia na mchezo huo dhidi ya Mtibwa.

“Nimewaandaa wachezaji kisaikolojia, lakini pia tumejipanga kucheza katika viwanja vibovu na kukabiliana na mazingira yote ili ushindi upatikane.

“Tumejiimarisha vyema kuhakikisha tunapata ushindi katika viwanja vya mikoani licha ya kwamba miundombinu yake haipo vizuri,” alisisitiza Zahera.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*