Yanga wamgeuka Waziri Mwakyembe

NA HUSSEIN OMAR

KLABU ya Yanga imeendelea kuikomalia Serikali ikitaka kusimamia uchaguzi wao wenyewe badala ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama ilivyoagizwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe.

Serikali kupitia Waziri Mwakyembe, iliiagiza uchaguzi wa Yanga kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kuwa klabu hiyo haina kamati ya kuratibu mchakato huo baada ya wale walioteuliwa kwa mujibu wa katiba, kukosa sifa.

Agizo hilo kuna wakati lilipingwa na baadhi ya wanachama wa Yanga, lakini baadaye ilidaiwa suala hilo lilimalizwa na kufikiwa makubaliano ya kufuata maelekezo ya Serikali.

Lakini wakati wadau wa soka nchini wakijiandaa kushuhudia Yanga ikipata viongozi wapya, jana Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya klabu hiyo, George Mkuchika, alitangaza kutokubaliana na msimamo wa Serikali.

Akizungumza kwenye makao makuu ya Yanga, Jangwani, Dar es Salaam, baada ya mazungumzo ya muda mrefu juu ya uchaguzi wa klabu hiyo, alisema wamekubaliana kubadilisha tarehe ya uchaguzi.

“Tumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu juu ya uchaguzi wa Yanga… tumekubaliana kwamba tubadilishe tarehe ya mkutano wa uchaguzi mkuu wa Yanga.

“Kwa mujibu wa katiba yetu, uchaguzi mkuu wa Yanga unatakiwa kufanyika mwakani. Baraza la Wadhamini limezingatia kwamba mwakani kuna uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na rais, tumeona si busara kufanya uchaguzi mkuu mwakani.

“Kwa hiyo tumekubaliana na tunapendekeza uchaguzi huo ufanyike mwaka huu, tena uwe mkutano mkuu wa kujaza nafasi zote,” alisema Mkuchika.

Alisema kwa kuwa Yanga haina uongozi baada ya kujiuzulu kwa mwenyekiti na makamu mwenyekiti wao, wakati wajumbe wa kamati ya utendaji wakiwa wamebaki wachache, watalazimika kuitisha mkutano mkuu wa wanachama kwanza ili kupata ridhaa yao juu ya azimio lao hilo.

Previous Article

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*