YANGA NJAA KWISHA

*Mashabiki waishio ughaibuni wacharuka katika kuichangia timu yao

*Wasema wamechoka kubezwa na Simba, Dola za Marekani zazidi kumiminika Jangwani

NA TIMA SIKILO

MAMBO yamezidi kupamba moto Yanga kwani wadau wa klabu hiyo wameendelea kuichangia ili kukabiliana na changamoto ya kifedha inayowakabili kiasi cha kushindwa kulipa mishahara na posho za wachezaji.

Wiki iliyopita, Kocha Mkuu wa Yanga, Miwnyi Zahera, alitinga ofisi za BINGWA na DIMBA zilizopo Sinza Kijiweni, Dar es Salaam, kuwasilisha kilio chake kwa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuichangia ili msimu ujao aweze kusajili kikosi cha ‘kufa mtu’ tayari kutoa upinzani wa kweli kwa watani wao wa jadi, Simba.

Zahera ni miongoni mwa wadau wa soka hapa nchini wanaokiri ubora wa kikosi cha Simba, akiamini iwapo atapata fedha za kutosha, anaweza kusajili wachezaji wa kiwango cha juu ambao wanaweza kukabiliana na nyota wa Wekundu wa Msimbazi hao.

Mara baada ya ziara yake hiyo, wadau wa Yanga waishio nchi za Marekani, Uingereza, Ubelgiji, Sweden, Denmark na kwingineko wanaounda kundi la mtandao wa kijamii ‘group’ wa Whatsapp lililopewa jina la Yanga wa Ughaibuni, walianza mara moja kuichangia timu yao.

Na baada ya kuona habari juu ya uamuzi wao huo zimechapishwa katika gazeti la BINGWA wiki iliyopita, wadau hao wa Yanga walizidi kupandwa na mzuka na kuendelea kuhamasishana kuipiga tafu klabu yao hiyo.

Hadi jana mchana, wadau zaidi wa klabu hiyo na wengine wakiwa ni mashabiki wa Simba, walikuwa wameichangia Yanga zaidi ya Dola za Marekani 500, huku wengine wakiahidi kuchangia  ndani ya mwezi huu.

Akizungumza na BINGWA kutoka Marekani, kiongozi wa kundi hilo, Luke Joe, alisema baada ya kusikia kilio cha Zahera kupitia BINGWA, waliamua kuanza mara moja kuchangishana wakiahidi kuendelea kuisaidia timu yao hiyo ili kukabiliana na ukata unaoitesa klabu hiyo.

“Tulianza kuchangia wiki iliyopita na tulipoona habari yetu imechapishwa katika gazeti lenu, wengi tumehamasika sana kuendelea kuichangia timu yetu ya Yanga.

“Tumekuwa tukihamasishana kuisaidia Yanga yetu kila tunapokutana kwenye sehemu za starehe, makazini na kwingineko. Wengi wameitikia wito na kuanza kutuma michango yao, watu wanachanga kuanzia dola 20, 30 hadi 50 kutegemea na hali ya kila mmoja.

“Nimhakikishie kocha Zahera, hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Machi, tutakuwa tumechanga fedha za kutosha, tunamwomba azidi kufanya kazi kwa bidii sisi tupo nyuma yake. Kimsingi tunamkubali sana huyu kocha ndio maana tumeamua kuungana naye kumsapoti katika jitihada zake za kuisuka upya Yanga,” alisema Joe.

Alisema mwishoni mwa mwezi huu, fedha zote watakazokuwa wamezichanga, wataziingiza katika akaunti ya Yanga ya CRDB ambayo inasimamiwa na Zahera na nahodha wa timu hiyo, Ibrahim Ajib na kwamba risiti itatumwa kwa kocha huyo na wachezaji wa klabu hiyo kwa ujumla.

Joe aliwataja wadau wa Yanga waishio ughaibuni walioichangia klabu hiyo hadi jana mchana kuwa ni yeye mwenyewe, Deo Ngassa, Ebra NY, Eleonora Heiland, Ibrahim Selungwi, Kessy Ernest, Kinyasi Monyi, Dulla Riyami, Abdullah Mohammed na Tino Malinda.

Wengine ni Patrick Kajale, Alberto Othuon, Dullah Mwanakatwe, Hassan Diwani, Edwin Waluye, Rehema Sarmett, Muli Chomba, Liga Hamza, Arthur Chipweli, Rebecca Ndekeja, Tito Kalumanga, Ally Idowa, Ntimi Joseph, Abdull Kufakunoga, Asha Hariz, Alu Nyang’oro na Stephen Tomy.

Juu ya mpango huo, Zahera alisema kuwa hiyo ndiyo njia pekee ya kuiwezesha Yanga kuitia presha Simba msimu ujao, lakini pia kufanya makubwa katika michuano ya kimataifa.

Zahera anaamini kuwa Yanga haiwezi kusajili mchezaji wa kiwango cha juu kukabiliana na timu kubwa Afrika iwapo haitakuwa na fedha za kutosha.

Alisema wachezaji wengi wa kiwango cha juu, hugombaniwa hivyo ili timu iweze kuwapata, huhitaji kuwa na fedha za kutosha kwa ajili ya usajili na mishahara.

“Yanga kuna wachezaji ambao lazima watoke ili tuweze kusajili wengine wa kiwango cha juu ambao ili uwapate, lazima uwe na fedha.

“Kwa kuwa shauku yangu ni kufanya vizuri zaidi msimu ujao, lazima niwe na wachezaji wa kiwango cha juu, zaidi ya hapo, itakuwa ni sawa na kupoteza muda na hakutakuwa na sababu ya mimi kuendelea kuwepo Yanga,” alisema.

Alisema kwa kutambua hilo, ndio maana ameanzisha mpango wa mashabiki na wanachama wa Yanga kuichangia timu yao ambao hata hivyo amebaini umekuwa ukisuasua mno.

“Kama kila shabiki na mwanachama wa Yanga angechanga Sh 2,000, kwa watu milioni moja, zitapatikana Sh bilioni mbili ambazo zinatosha kabisa kulipa madeni ya wachezaji na kusajili wachezaji wengine wapya wa kiwango cha juu kwa ajili ya msimu ujao,” alisema.

Aliongeza: “Nikipata kiasi kama hicho (Sh bilioni 2), Yanga itasumbua sana msimu ujao kwani itakuwa na kikosi cha kutisha. Sitaki niteseke msimu ujao, kama hali itakuwa hivi hivi, ni heri niondoke kuliko kuendelea kuumiza kichwa na kupata ushindi kwa jasho.”

Zahera aliwataka mashabiki na wanachama wanaoipenda Yanga kuichangia kupitia akaunti ya CRDB au NMB kwenda namba 015419775800 ambapo jina la akaunti ni Yanga Collection au kwa kutumia TigoPesa, watume kwenda namba ya kampuni 101120, jina litakalotokea ni Yanga.

Pamoja na kukabiliwa na hali ngumu kifedha, Yanga imeendelea kuongoza Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa imejikusanyia pointi 67 kutokana na mechi 27.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*