Yanga, JKT, Panana zatoa vipigo SWPL

NA GLORY MLAY

TIMU ya soka ya Yanga Princess imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Marsh Academy Sport, katika mchezo Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (SWPL), uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa ushindani huku timu zote zikishambuliana ambapo katika dakika ya kwanza Yanga ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Thabea Aidano, baada ya kumalizia mpira uliopigwa na Flora Kayanda.

Timu hizo ziliendelea kushambuliana kwa kasi na dakika ya 34, Aisha Juma, aliipatia Yanga bao la pili baada ya kupiga shuti lililozama moja kwa moja nyavuni.

Hata hivyo, Marsh Academy walifanikiwa kupata bao dakika za nyongeza kipindi cha kwanza kupitia kwa Editha Mwela, aliyemalizia mpira wa kona.

Kipindi cha pili kilianza huku kila timu ikisaka nafasi ya kufunga ambapo dakika ya 46 Yanga waliongeza bao la tatu kupitia kwa Thabea baada ya kupiga shuti lililozama wavuni.

Dakika ya 87, Marsh walicharuka na kufunga bao la pili kupitia kwa Yasinta Peter, aliyepiga mpira wa kona uliojaa moja kwa moja nyavuni.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Panama waliibuka na ushindi wa mabao 3 -0 dhidi ya Mapinduzi Queens kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.

Vinara wa ligi hiyo, JKT Queens nao waliichapa Tanzanite ya jijini Arusha mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*