Wasanii wa kiume wavaa hereni wanavyowakera viongozi wa dini

BRIGHITER MASAKI

KWA kawaida, hereni ni miongoni mwa mapambo yaliyokuwa yamezoeleka kuvaliwa na wanawake kama sehemu ya kuongeza urembo na mvuto wao kwa ujumla.

Wanawake wengi tangu zamani, pamoja na kujipodoa kwa manukato mbalimbali, wamekuwa wakivaa hereni masikioni mwao wakiamini mapambo hayo yanawaongezea kitu na kuwa na mvuto mbele ya wenzao.

Hata hivyo, si wanawake wote ambao wamekuwa wakivaa hereni, wengine wamekuwa wakitumia mapambo mengineyo kama bangili, shanga, vipini vya puani na kadha wa kadha.

Kwa siku za hivi karibuni, hereni zimetokea kuwabamba na wanaume, hasa vijana mastaa wa fani mbalimbali kuanzia muziki, filamu, uanamitindo na nyinginezo.

Miongoni mwa wasanii wa kiume ambao wamekuwa wakivaa hereni ni Juma Mussa ‘Jux’, Naseeb Abdul ‘Diamond’, Raymond Mwakyusa ‘Rayvanny’, Rajab Abdul ‘Harmonize’, Baraka Andrew ‘Baraka Da Prince’ na wengine wengi.   

Kitendo cha wanaume kuvaa hereni na wakati mwingine kuvaa shanga miguuni (kikuku), kimekuwa kikiwagawa mashabiki wao na jamii ya Watanzania kwa ujumla.

Wengine wamekuwa wakilaani kitendo hicho wakiamini kinakiuka maadili ya Mtanzania, lakini pia ikiwa ni mfano mbaya kwa jamii inayomzunguka msanii husika, hasa watoto wa kiume.

Unapowauliza wanaume hao wenye tabia za kuvaa hereni, watajitetea kuwa ni sehemu ya fasheni inayolenga kuwafanya kuonekana watanashati zaidi.

Lakini wengi wamekuwa wakiamini kuwa tabia hizo zinatokana na ulimbukeni wa vijana wa Kitanzania kuiga tamaduni za kigeni, maana tumeona mastaa wengi wa nchi za Ulaya na Amerika hasa Marekani, wakiwa wamebobea katika aina hiyo ya urembo.

Katika mikusanyiko ya wasanii 10 wa kiume wa muziki na sanaa nyinginezo wa Marekani, huwezi kuwakosa saba wakiwa wamevaa hereni au hata kipini cha puani.

Kwa wasanii na jamii ya nchi hizo, hilo si jambo la kushangaza, wao wanaona ni kawaida tu lakini si kwa hapa Tanzania ambako pambo la hereni, shanga au kipini cha puani, zimezoelekea kwa wanawake tu.

Wapo wapenzi na wadau wa sanaa ambao wamekuwa wakishambulia kwa maneno wasanii wanaokiuka maadili ya Kitanzania, wakiwamo wale wanaovaa hereni na vidani vinginevyo vilivyozoeleka kwa wanawake, wakiwataka kuachana na tabia hiyo bila mafanikio.

Katika kuonyesha jinsi tabia hiyo inavyowakera wengi, hatimaye baadhi ya viongozi wa dini wameamua kuwatolea uvivu wasanii wavaa hereni na vidani vingine vya kike.

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC), lililopo Ubungo Kibangu, jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, wakati wa mkesha wa Mwaka Mpya 2019, alikuwa akieleza kile alichokiita ni ‘ujinga’ wa mastaa wa kiume wa tasnia ya Bongo Fleva na Bongo Movie kuvaa hereni.

Alidai kwamba siku chache kabla ya mafundisho yake hayo, alikutana na mastaa wa tasnia hizo na alishangazwa kuwaona wakiwa wamesuka nywele, kuvaa hereni na kuvaa suruali chini ya makalio.

“Miaka ya 1970 wakati ninakua, mwanaume au kijana wa kiume ukisuka nywele, mama yako atatafuta mtaa wa kwenda kuishi. Atafukuzwa mtaani kama mbwa koko (mbwa anayerandaranda ovyo), siyo kijana mwenyewe, lakini yeye na mama yake watafukuzwa kama mbwa koko.

“Kule kwetu Iringa, tulikuwa na watu walioitwa wahindi koko na mbwa koko. Ilikuwa kijana wa kiume ukivaa hereni, hata shule unayosoma ulikuwa unafukuzwa kama mbwa koko.

“Leo, eti ili uonekane wewe ni supastaa ni lazima uvae hereni na kusuka nywele na Basata (Baraza la Sanaa la Taifa) lipo na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo.

“Huo ni ujinga, kwani hawa vijana wanakua. Mimi huwa ninajiuliza, kijana ambaye leo anavaa hereni, hajui kuna maumivu ambayo wazazi wake wanayapata kuwa na kijana wao?” alihoji Mzee wa Upako.

Aliongeza: “Inafika usiku dume zima unaanza kufumua nywele…mke au dada yako anafumua nywele na wewe unafumua nywele! Mke wako au dada yako anavua hereni na wewe kijana wa kiume unavua hereni!

“Huo utamaduni wa wapi kama si upuuzi? Kijana ambaye leo anavaa hereni, maumivu ambayo wazazi wake wanayapata kuwa na kijana wao wa kiume anayevaa hereni, atayapata kijana huyo siku mtoto wake wa kiume atakapokuwa amevaa hereni kwani mtoto wa nyoka ni nyoka.

“Ningekuwa nina uamuzi katika Serikali, kijana yeyote wa kiume, mwanamuziki au mwigizaji wa sanaa, filamu yake au wimbo wake nisingeupitisha kama huwa mhusika anavaa hereni au anasuka nywele.

“Kusuka nywele na kuvaa hereni ni ishara za ushoga, kuna roho wa ushoga anawatafuta watu wetu. Hii si salama hata kidogo, kuna roho wa uovu anawaandama bila wenyewe kujua.”

Hata hivyo, wapo wasanii ambao pamoja na kuwa mastaa wa kutupwa, lakini wamekuwa wakiheshimu utamaduni wa Mtanzania kwa kujiweka mbali na mapambo yaliyozoeleka kwa wanawake kama hereni na mengineyo.

Wasanii hao ni Ben Pol, Profesa Jay, Sugu, Ali Kiba, AY, Mwana FA, Nikki wa Pili, Roma na wengineo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*