WANATOKA

W*Solskjaer apanga kufanya maajabu Camp Nou, kocha Barca ampiga kijembe

*Ajax ‘full’ mzuka unaambiwa, Juve kukomaa mwanzo-mwisho

CATALUNYA, Hispania

USIKU wa Ulaya umerejea tena, moto ni uleule katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa vigogo wa nchini England, Manchester United, kushuka uwanjani leo watakapokuwa wageni wa Barcelona.

Wiki iliyopita timu hizo zilipokutana, Barcelona walifanikiwa kushinda bao 1-0 katika Uwanja wa Old Trafford baada ya beki wa Manchester United, Luke Shaw, kujifunga.

Huku mchezo wa pili ukichezwa katika Uwanja wa Juventus kati ya Juventus na Ajax, baada ya mchezo wa kwanza kumalizika kwa sare ya bao 1-1 nchini Uholanzi.

Lakini kuelekea kwenye michezo hiyo, kumekuwa na tambo nyingi baada ya kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer, kuwapiga ‘biti’ Barcelona na kuwaambia kuwa wasitegemee kupata mteremko kabisa.

Tena akiwataka kuwa makini, kwani ana kikosi cha wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuharibu mtiririko wao wa ushindi walioupata hivi karibuni.

“Michezo kadhaa iliyopita tulifanya vibaya na kuweka nafasi ya ‘top four’ katika mazingira magumu, lakini hilo halitufanyi tushindwe kupata ushindi dhidi ya timu bora kama Barcelona.

“Valverde ni kocha bora duniani mwenye mbinu nyingi za mchezo, tupo tayari kupambana bega kwa bega kuhakikisha tunashinda kesho (leo),” alisema Solskjaer.

Hata hivyo, Barcelona tangu kuanza kwa msimu huu, wamekuwa na rekodi nzuri ya kupata matokeo ya ushindi katika uwanja wao wa nyumbani wa Camp Nou.

 “Kila mmoja yupo tayari kupambana kwa ajili ya timu hii, bado Manchester United ni klabu ya kuogopwa hasa kama utakumbuka walichokifanya dhidi ya PSG.

“Pengine ni nafasi ya kipekee msimu huu kwa Barcelona kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, hatuwezi kupuuzia mchezo huo kwa kuwa tulishinda wa kwanza,” alisema kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde.

Mchezo mwingine mkali utakuwa kati ya Juventus na Ajax, mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1 huku Cristiano Ronaldo na David Neres wakizifungia timu zao.

Pamoja na Ajax kutoa upinzani mkubwa katika mchezo wa kwanza, kocha wa Juventus, Masimilliano Allegri, amesema wapinzani wake wajipange kukutana na mechi kali ya ushindani.

“Ajax ni timu nzuri, wana vijana ambao wanakupa picha jinsi gani watakuwa miaka kadhaa ijayo, wategemee kuiona Juventus tofauti.

“Tunataka kushinda mchezo huo ili twende nusu fainali, ikiwezekana fainali na kushinda taji hilo,” alisema kocha huyo raia wa Italia.

Mikwara hiyo ilijibiwa na kocha wa Ajax, Erik ten Hag ambaye amesema bado kikosi chake hakijamaliza kazi walioifanya nchini Uholanzi.

“Juventus ni timu ngumu lakini hakuna linaloshindikana kama tukicheza kwa ushirikiano, tutashinda kama tutatumia nafasi zetu vizuri na kuwazuia wasilete madhara kwetu,” alisema Hag.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*