WAKIIVAA AL AHLY KESHO… Simba wala kiapo

*Wachezaji waahidi kucheza kufa au kupona, Mo Dewji awapandisha mzuka

NA ZAITUNI KIBWANA

WACHEZAJI wa Simba wameapa kucheza kufa au kupona kuhakikisha wanaifunga Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba SC watakuwa wenyeji wa Al Ahly katika mchezo huo wa marudiano wa Kundi D, ikiwa ni baada ya Wekundu wa Msimbazi hao kukubali kipigo cha mabao 5-0 walipokuwa ugenini mjini Alexandra, Misri wiki iliyopita.

Kuelekea mchezo huo, Simba watatakiwa kupata ushindi wowote ule ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Ni kutokana na kutambua hilo, uongozi wa Simba pamoja na benchi la ufundi la timu yao, wameweka mikakati kabambe kuhakikisha Al Ahly hawatoki Uwanja wa Taifa.

Mwekezaji wa klabu hiyo, bilionea Mohammed Dewji ‘Mo’, tayari ametamba timu yao lazima ishinde kesho, akiwataka wachezaji wao kupambana kwa nguvu na uwezo wao wote ili kuwapa raha mashabiki wao.

Aliwataka mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho ili kuwasapoti vijana wao waweze kupata ushindi, akiamini uwezo wa kutinga robo fainali wanao iwapo watavuna pointi tatu dhidi ya wapinzani wao hao na baadaye AS Vita ya DR Congo itakapokuja nchini.

Kwa upande wa wachezaji wa timu hiyo, wameweka wazi jinsi watakavyopambana kesho ili kuwafuta machozi mashabiki na viongozi wao.

Wakizungumza na BINGWA jana, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi, Pascal Wawa na Jonas Mkude wote wameahidi kutoa kipigo kikali kwa Al Ahly, huku wakiomba Mungu waamke salama siku ya mchezo huo.

“Tunacheza dhidi ya timu ngumu Afrika, tumejifunza kilichotokea Misri na Kongo (DRC), sasa hatutaki kuona kinajirudia hapa nyumbani,” alisema Mkude.

Wawa, raia wa Ivory Coast yeye alisisitiza: “Tutapambana mpaka hatua ya mwisho kupata matokeo, tunajua tumefungwa mabao 5-0, ni mengi ila tumejifunza na hatutarudia makosa.”

Okwi yeye alisema: “Tupo vizuri, siwezi kusema tumejiandaa vipi au tunafanya nini, watu waelewe tu kazi tutaifanya keshokutwa (kesho) Uwanja wa Taifa.”

Niyonzima aliongeza: “Ni mechi ngumu ambayo inahitaji uzoefu kidogo, endapo nitapewa nafasi ya kuanza kuna kitu ambacho ninaweza kuwafanyia Simba.’’

Kikosi cha Simba kimejichimbia katika Hoteli ya Sea Scape iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam kujiandaa na pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa.

Simba sasa wapo nafasi ya tatu kwenye kundi lao wakiwa na pointi tatu, wakati Ahl Ahly ni vinara na alama zao saba, huku AS Vita ikiwa ya pili na pointi zao nne na JS Saoura wakishikilia mkiani na alama zao mbili.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*