Wadau, wanamuziki wa dansi jiongezeni kwenye hili

CHRISTOPHER MSEKENA
KATIKA vilinge mbalimbali vya muziki wa dansi hapa Tanzania si jambo la ajabu sana kukuta mijadala yenye hoja kuhusu uhai na kifo cha muziki huo hasa kipindi hiki ambacho Bongo Fleva imeshika hatamu.

Mijadala hiyo inapata nafasi kutokana na ukweli kwamba mambo yanayoongeza hamasa kwa mashabiki kufuatilia dansi yamepungua kwa kiasi kikubwa kwenye vichwa vya habari za burudani na zaidi kutawaliwa na wasanii wa Bongo Fleva na Bongo Movie.

Licha ya dansi kuonekana imepoteza mvuto na haina maajabu tena kwa mashabiki, wanamuziki wake wameendelea kuzalisha muziki kila uchwao japokuwa changamoto ni namna bidhaa hiyo (nyimbo) inavyoweza kuwafikia walaji (mashabiki).

Vyombo vingi vya habari hasa redio na runinga hazina vipindi vyenye maudhui ya dansi. Vipindi vingi vinatumia muziki wa Bongo Fleva saa 24 kwa siku 6 angalau redio na runinga nyingine hutenga siku moja wikiendi kwa kucheza muziki wa dansi kwa saa 2.

Kwa mfumo huo, dansi inalazimika kuwa muziki wa nyongeza ndiyo maana unaonekana umepotea kwa kuwa haupewi nafasi kubwa ya kuchezwa na kuzungumziwa kama vile wasanii wa Bongo Fleva na muziki wao wanavyopata nafasi hiyo.

Hivyo basi mwanamuziki au bendi ya dansi ikitengeneza kazi mpya inakuwa ngumu kukufikia wewe shabiki, nyimbo zinafanyika ila haziwafikii kwa wakati mashabiki wa dansi na hata zikiwafikia watazisikia na kuziona mara chache kwenye redio na runinga.

Kwa muktadha huo basi, nina machache kwa wadau, wanamuziki na mashabiki wa dansi nchini ili tuweze kutoka hapa tulipokwama maana naamini dansi ina mashabiki wengi na wasanii ndio wenye jukumu la kurudisha morali iliyopotea.

Kwanza kabisa huu si muda wa wanamuziki kutegemea redio na runinga kufikisha muziki wao kwa mashabiki. Vyombo vingi vya habari vinaendeshwa kibiashara hivyo kila dakika kwao ni fedha, sasa ngoma zetu za dansi ili zinoge angalau zipigwe dakika 5 hivi.

Sasa usitarajie wimbo wako uchezwe redioni au runingani kwa hizo dakika zote. Ni vizuri wanamuziki binafsi wa dansi na bendi kuwekeza nguvu nyingi kwenye mitandao ya kijamii kwani huko ndiko biashara ya muziki inafanyika.

Natamani kuona wasanii wengi wakiwauzia mashabiki zao nyimbo kupitia mkito.com, boomplaymusic, wasafi.com, deezer, sportfy na sehemu nyingine ambazo zinawaingizia fedha nyingi wasanii wa Bongo Fleva. Wanamuziki wa dansi acheni kutegemea maonyesho ya mwisho wa wiki.

Pia huu ni muda wa kutengeneza nyimbo zinazoenda na wakati. Nyimbo ndefu ni kama zimepitwa na wakati, zinakera na kuchosha si rahisi mtu akasikiliza mwanzo mwisho, tutengeneze nyimbo fupi, tamu zilizojaa vionjo na ubunifu wenye kukonga nyoyo.

Hakuna kinachoshindikana ni sisi wenyewe wana dansi kuamua kufanya mabadiliko haya, mashabiki wapo tayari kupokea chochote kizuri kutoka kwa wanamuziki ila matatizo ya kufanya kazi kimazoea ndiyo yanarudisha nyuma muziki huu pendwa kusonga mbele.

Mwisho wanadansi tunachukiana na kunyimana michongo wakati wenzetu huko Bongo Fleva na Bongo Movie wanashikana mikono na kusapotiana katika kila hatua wanayopiga ndiyo maana wanasonga mbele, tubadilike.

NUKUU

“Unavyozidi kukua ndiyo matatizo yanazidi kukuzonga zaidi ya jana, unaweza amini kuwa ukiwa na pesa basi matatizo yako yanaweza kupungua kumbe hapana wakati unazidi kuwa na pesa ndipo matumizi ya pesa huongezeka zaidi,”

Ali Kiba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*