Verratti, Cavan kuikosa Man Utd

PARIS, Ufaransa

KOCHA Thomas Tuchel amesema huenda asiwe na nyota wake, Marco Verratti na Edinson Cavani, katika safari ya timu ya Paris Saint-Germain kwenda kuivaa Manchester United katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya 16 bora itakayopigwa kesho.

Cavani ndiye aliyefunga bao pekee katika mchezo wa juzi ambao PSG waliibuka na ushindi dhidi ya Bordeaux, lakini hakuweza kuumaliza mtanange huo kwa kile kinachodaiwa ni matatizo ya misuli ya nyama za paja.

 Nyota huyo ni kati ya wachezaji walioanzishwa kikosi cha kwanza cha PSG baada ya Tuchel kuwaweka benchi nyota wake kama vile, Leandro Paredes  na Kylian Mbappe kwa ajili ya mechi hiyo itakayopigwa katika dimba la Old Trafford.

PSG tayari imeshamkosa nyota wake mwingine tegemeo, Neymar na Tuchel anakiri akisema kwamba, Cavani ataikosa mechi hiyo jambo ambalo litakuwa ni pigo kubwa kwa mabingwa hao wa Ligue 1 watakaoikabili Man United ambayo inaonekana kuwa moto wa kuotea mbali, baada ya kushinda mechi 10 kati ya 11 tangu ianze kunolewa na kocha wa muda, Ole Gunnar Solskjaer.

“Kwa sasa tulikuwa na mkakati B,” aliwaambia waandishi wa habari. “Bila kuwapo Neymar, pengine hatakuwapo  Marco ama Cavani, sasa tunatakiwa kuwa na mkakati D,” aliongeza kocha huyo.

“Kwa sasa siwezi kusema kuwa tuna mipango mingi tofauti, tunapaswa kwanza tuiangalie  Manchester United, hivyo tunatakiwa kuwa wapole na kujiamni,” alikwenda mbali zaidi kocha huyo.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*