USIJIDANGANYE…Yanga, Simba bado ngoma mbichi kabisa

NA AYOUB HINJO

KAMA ilivyo kwa mashabiki wa Ulaya na Amerika wanavyojivunia michezo mikubwa pindi timu wanazoshabikia zinapokutana na kuwa stori kubwa kwao.

Basi hata katika Bara la Afrika nako hakuna tofauti na Ulaya au Amerika, ambako huaminika kuna mashabiki vichaa wa soka kuliko kwingine kokote katika kona ya dunia hii.

Mara nyingi timu inayoshinda katika mchezo huo, mashabiki wake huwa na nafasi kubwa ya kutawala eneo husika kwa furaha na kufikia hatua ya kufanya sherehe.

Mapema joto la mchezo wa Simba na Yanga limepanda hata kabla ya mechi husika kuchezwa, Jiji la Dar es Salaam limegawanyika mara mbili kutokana na timu hizo kuwa na mashabiki wengi katika kila kona ya nchi ya Tanzania.

Pia, hata nchi jirani huwa na shauku kubwa ya kushuhudia pambano hilo kwa kufunga safari mpaka Tanzania ili kuona jinsi mtanange huo unavyokuwa.

Mchezo wa watani wa jadi hapa nchini unazidi kuteka hisia za wadau wa soka kadiri siku zinavyokwenda huku mashabiki wa timu za Simba na Yanga, wakitambiana kuibuka na ushindi hapo Jumamosi.

Mchezo huo wa watani wa jadi upo ndani ya tano bora ya zile ‘derby’ kali za Afrika, huku nyingine zikiwa Al Ahly dhidi ya Zamalek (Misri), Orlando Pirates dhidi ya Kaizer Chiefs (Afrika Kusini), Club Africain wanapokutana na Esperance Sportive (Tunisia) na Wydad Casablanca na Raja Casablanca (Morocco).

Makala haya yanakuletea uchambuzi wa kila timu, yaani udhaifu na ubora wao ulipo na kipi kifanyike ili zipate matokeo ya ushindi ikiwa mchezo huo unatazamiwa kutoa mwanga wa bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

SAFU YA ULINZI

Tofauti na Simba ambao kwa kiasi kikubwa nafasi ya mlinda mlango husimama Aishi Manula, Yanga mpaka sasa wametumia walinda mlango watatu tofauti, Beno Kakolanya, Ramadhan Kabwili na Klaus Kindoki, bado haijajulikana ni yupi anasimama dhidi ya Simba leo.

Lakini ngome hiyo imekuwa ikipitika kwa urahisi na wapinzani huku mlinda mlango akifanya kazi ya ziada, mara zote huonekana wakifungwa mabao mepesi ambayo yanatokana na mawasiliano hafifu kati yao.

Ngome ya ulinzi ya Yanga inaongozwa na beki mzoefu, Kelvin Yondani anayesaidiwa na Andrew Vincent, Gadiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na chipukizi Paul Godfrey aliyechukua nafasi ya majeruhi, Juma Abdul kikosini.

Mpaka kufikia sasa, Simba wamefanikiwa kucheza michezo 15 ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa nyuma/ pungufu kwa michezo nane dhidi ya Yanga waliocheza 23.

Lakini ndani ya michezo hiyo wamefanikiwa kufungwa mabao matano, lakini mpaka sasa wamefungwa mchezo mmoja, walikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Mbao ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ukuta wa Simba unaongozwa na kipa, Aishi Manula anayelindwa na Jjuuko Murshid, Pascal Wawa, Zana Coulibaly, Nicolas Gyan, Mohamed Hussein na Asante Kwasi, wanaobadilishana nafasi hiyo ya beki wa kushoto.

Udhaifu mkubwa unaoonekana ndani ya safu hiyo ya ulinzi ni kuruhusu kufungwa mabao ya mipira ya kutengwa (faulo na kona), wachezaji hushindwa kujipanga vizuri kuwakabili wapinzani wao.

Safu ya ulinzi ya Simba inaonekana kuwa bora zaidi ya watani wao ambao katika michezo 23 waliyocheza wamefungwa 15.

SAFU YA KIUNGO

Moja ya maeneo yanayotazamwa na wengi ni vita ya eneo la kiungo kwa timu zote mbili, wakiongozwa na viungo wenye uwezo mkubwa wa kusakata kabumbu.

Tangu kuanza kwa msimu huu, Yanga wamekuwa wakitumia wachezaji tofauti katika eneo hilo la kiungo lakini Feisal Salum ‘Fei Toto’ ni mchezaji tegemeo kwenye eneo hilo akiwa na kazi ya kuisukuma timu hiyo kwa pasi zake kutokea chini.

Lakini bado wapo akina Papy Tshishimbi, Pius Buswita na wengine ikiwa wakati mwingine kocha wa kikosi hicho, Mwinyi Zahera, humtumia Ninja kwenye eneo hilo ili kutibua mipango ya wapinzani wao.

Hata hivyo, kwa dakika zote 90 za mtanange huo watakuwa na kibarua cha kukabiliana na viungo wa Simba, akiwamo Mkude ambaye kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi ndiye mfalme wa eneo hilo.

Pia, mashabiki wa Yanga wanajivunia uwepo wa Ibrahim Ajib, ambaye hivi karibuni amekuwa katika kiwango cha juu kwa kutoa pasi zaidi ya 10 za mabao huku akifunga zaidi ya matano katika michezo aliyocheza.

Kwa namna moja au nyingine matokeo ya ushindani kwa timu yoyote kati ya hizo itategemea na jinsi viungo wao watafanya kitu gani uwanjani.

Uwepo wa Jonas Mkude, James Kotei, Clatous Chama, Mohamed Ibrahim, Said Ndemla, Hassan Dilunga na wengine unampa machaguo mengi kocha wa kikosi hicho ikiwa tayari eneo la kiungo la Simba kuonekana kuwa na ushindani mkubwa wa nafasi.

Katika michezo ya hivi karibuni, Mkude na Kotei wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwa pamoja wanapocheza kama viungo wakabaji ‘double holding’ huku Chama akipandisha mashambulizi na kupeleka mipira kwa washambuliaji wao.

SAFU YA USHAMBULIAJI

Moja ya maeneo yanayofanya mashabiki wa timu zote mbili wajivunie timu zao basi ni safu ya ushambuliaji kuongozwa na wafumania nyavu matata.

Licha ya Simba kutajwa kuwa na washambuliaji wenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao, lakini hawajafanikiwa kufua dafu mbele ya wapinzani wao.

Aidha, Yanga ambao hawakupewa nafasi kubwa tangu kuanza kwa msimu huu wamefanikiwa kufunga mabao 40 katika michezo 23 waliyocheza, tena wakiwa timu pekee iliyofunga mabao mengi licha ya kuwazidi Simba kwa michezo nane.

Huku straika wa kikosi hicho, Heritier Makambo, akiongoza kwa ufungaji mabao ndani ya timu hiyo, amefunga mabao 11, Ajib akiziona nyavu za wapinzani mara sita.

Makambo na Amisi Tambwe wanasifika kwa kufunga mabao ya vichwa lakini ni wachezaji wenye uwezo wa kupenya ngome ya wapinzani kwa pasi kutoka kwenye eneo la kiungo.

Wakati mwingine, hufunga mabao yao kwa mashuti makali ambao katika michezo kadhaa mabao ya aina hiyo yaliamua matokeo ya ushindi kwao.

Katika michezo 15 Wekundu wa Msimbazi waliyoshuka dimbani, wamefanikiwa kuziona nyavu za wapinzani wao mara 31, huku kinara wa kupachika mabao ndani ya timu hiyo akiwa ni straika, Meddie Kagere aliyefunga mara nane akifuatiwa na Emmanuel Okwi mabao saba.

Nyota watatu wanaoiongoza timu hiyo kwenye eneo la ushambuliaji kila mmoja ana sifa yake anapokuwa mbele, John Bocco ana uwezo wa kufunga mabao ya vichwa kama ilivyo kwa Kagere.

Lakini Okwi mara nyingi huwa mjanja zaidi kwa kutumia uwezo wake wa kupangua ngome ya wapinzani kwa chenga na kupiga mashuti makali, mara nyingi wakianza wote watatu hutumika zaidi kwenye nafasi ya winga ili kutengeneza nafasi kwa wengine kwa kutoa pasi au kufunga mabao.  

ZAHERA v AUSSEMS

Unakuwa mchezo wa pili kuwakutanisha makocha hao baada ya ule wa kwanza kumalizika kwa suluhu huku Simba wakikosa nafasi nyingi za wazi kufunga mabao.

Zahera tayari ameiongoza Yanga kwenye michezo 23 na kufanikiwa kushinda mara 18, sare nne na kufungwa mara moja, amekuwa akisifika kwa mbinu nyingi za kuipanga timu yake.

Yanga wamekuwa hawachezi soka la kuvutia lakini wamekuwa wakipata ushindi katika michezo yao mingi waliyocheza mpaka sasa.

Nao Simba chini ya Mbelgiji Aussems, wamekuwa moto wa kuotea mbali kila wanaposhuka uwanjani, kocha huyo ameiongoza Simba mara 15 na kupata ushindi mara 11, sare tatu na kufungwa mmoja.

Amekuwa akisifika kwa soka safi, huku wachezaji wa kikosi hicho wakicheza kwa pasi nyingi kuelekea kwenye lango la wapinzani wao.

Licha ya klabu hiyo kufanya vizuri bado washambuliaji wanashindwa kutumia nafasi zinazotengenezwa vizuri lakini mara zote huwa hatari mbele ya lango la wapinzani wao.

Bado matokeo ya mchezo huo yatategemea zaidi mbinu za makocha hao kabla ya uwezo binafsi wa wachezaji kuamua mechi hiyo kubwa Afrika Mashariki na Kati.

Mchezo wa mwisho uliozikutanisha timu hizo ulionekana wa upande mmoja, Simba walitawala kwa kiasi kikubwa licha ya kumalizika kwa suluhu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*