Ushindi waisahaulisha Coastal kipigo cha 8-1

OSCAR ASSENGA, TANGA

KOCHA mkuu wa timu ya Coastal Union, Juma Mgunda, amesema ushindi walioupata wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye mechi ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara, umewabadilisha fikra za kufungwa mabao 8-1 na Simba.

Mgunda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga, ambapo bao la Coastal Union lilifungwa na Ayoub Lyanga.

Alisema ushindi kwenye mechi hiyo ulikuwa ni muhimu sana kwao, kwani kitendo cha kupoteza mechi yao iliyopita kwa idadi kubwa ya mabao wakiwa ugenini kiliwapa wakati mgumu.

“Niseme kwamba namshukuru Mwenyezi Mungu cha msingi wachezaji wangu wameondokana na fikra ya kuwaza kufungwa goli nane, badala yake sasa watafikiria ushindi waliopata wa bao 1-0,” alisema.

Alieleza haikuwa kazi rahisi kupoteza mechi kwa kufungwa mabao mengi kiasi hicho, halafu kuingia kwenye mechi na kuweza kushinda.

Aidha, alisema hatua ya kwanza aliyoifanya baada ya kutua jijini hapa akitokea Dar es Salaam, ni kuwaandaa wachezaji hao kisaikolojia ili waweze kuhakikisha wanafanya vema mechi zinazofuata kwenye michuano hiyo.

“Kwa kweli kwa vijana wangu ambao ndio mwaka wao wa kwanza kucheza Ligi Kuu, ilikuwa vigumu sana kukubali kipigo hicho cha mbwa mwizi, lakini kwa siku chache nilizungumza nao niliweza kuwabadilisha na kuweza kupata matokeo kwenye mechi hii,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*