Siri ya waamuzi kuboronga TPL yavuja

NA ZAINAB IDDY

WAKATI kukiwa na malalamiko ya waamuzi kuchezesha vibaya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara zinazoendelea, siri imefichuka kwamba kucheleweshwa kwa posho zao ndicho chanzo cha tatizo hilo.

Hivi karibuni timu zimekuwa zikitoa malalamiko kwa waamuzi waliopewa dhamana ya kuchezesha mechi za Ligi Kuu kutokana na kushindwa kutafsiri sheria 17 za soka.

Akitoa ufafanuzi kuhusu suala hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), Joseph Mapunda, alisema katika msimu huu kumekuwa na tatizo la waamuzi kutopewa posho zao kwa wakati hasa baada ya ligi kukosa mdhamini mkuu.

“Suala la kucheleweshwa kwa posho za  waamuzi limekuwa kubwa katika mzunguko wa pili, hili limechangiwa na ligi kutokuwa na mdhamini ambaye siku si nyingi atarejea na hali itakuwa nzuri.

“Mwisho wa mwezi uliopita niliitwa na Mtendaji wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi (Salum Chama), nikaelezwa kuhusu hali ya uchumi ilivyo hivi sasa, hivyo na mimi nikakutana na waamuzi kuwaomba wawe wavumilivu,” alisema Mapunda.

Hata hivyo, alieleza kuwa baadhi ya waamuzi hawatafsiri ipasavyo sheria 17 za soka kutokana na mapungufu yao wenyewe ya kushindwa kuifanyia kazi taaluma hiyo.

“Changamoto ya kutolipwa kwa wakati imeanza katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu, ambapo sababu kubwa ni kuyumba kwa uchumi wa TFF,” alieleza Mapunda.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*