Simba waitikisa Mara

NA MAREGESI NYAMAKA, MUSOMA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, jana walipokewa na umati mkubwa wa mashabiki wa timu hiyo walipokuwa wakiingia Mara, mjini Musoma kwa ajili ya mchezo wao wa leo dhidi ya Biashara United.

Umati huo wa mashabiki ulianza kujitokeza kwa wingi zaidi Bunda Mjini ambapo walijipanga barabarani wakidai wanasubiri timu hiyo tangu saa 12:00 asubuhi.

“Tupo hapa tangu saa 12:00 alfajiri kwa kuwa ni muda mrefu hatujaiona timu yetu,” alisema Ally Juma ambaye alilalamikia kitendo cha gari iliyoibeba timu hiyo kushindwa kusimama kwa ajili yao.

Gari hiyo aina ya Toyota Coaster yenye namba T457 DPU iliyobeba kikosi hicho cha Simba, ilipita eneo hilo la Bunda saa 5:00 asubuhi.

Shangwe hilo la mashabiki liliendelea hadi kwa mashabiki wengine wa Musoma ambapo ndipo utakapochezwa mtanange huo kwenye Uwanja wa Karume, msafara huo uliongozwa na pikipiki na gari la polisi kwa ajili ya usalama barabarani.

Simba watakutana na Biashara United leo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya KMC ya Kinondoni kwenye mchezo uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Wekundu hao wa Msimbazi watashuka dimbani wakiwa wanahitaji kuendeleza wimbi la ushindi ili waendelee kujiwekea matumaini ya kutetea ubingwa wao msimu huu.

Simba wako kwenye harakati za kuhakikisha wanatetea ubingwa huo wa Ligi Kuu ili warejee tena kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa hatua ya robo fainali na TP Mazembe.

Simba wamekuwa kwenye kazi nzito ya kucheza viporo vyao kila baada ya siku moja tangu walipotolewa ili waweze kulingana na wengine ambao tayari wamekwishafikisha mechi 32 na wao wakitarajiwa kucheza mechi ya 27 leo.

Kwa sasa Simba ambayo imecheza michezo 26 inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 66, wakiwa nyuma ya mahasimu wao Yanga wenye pointi 74 baada ya kucheza michezo 32.

Lakini Simba watakuwa na kazi ngumu kwa Biashara United ambao wako nafasi ya 19 baada ya kucheza mechi 34, kutokana na kuwa kwenye hatari ya kushuka daraja.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*