Sevilla wathibitisha safari ya Tanzania


MWANDISHI WETU

MABINGWA mara tano wa michuano ya UEFA Europa League, Sevilla, wamethibitisha kuja nchini kuvaana na timu ya Simba au Yanga.

Safari ya klabu ya Sevilla ambayo inashiriki Ligi Kuu Hispania maarufu La Liga, imewezeshwa na Kampuni ya michezo ya kubahatisha SportPesa.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya La Liga Kimataifa, Oscar Mayo, alisema mradi wa La Liga World Challenge unakusudia kupanua brandi ya La Liga duniani.

“Ni nafasi adimu kwa kila mtu kwamba mashabiki wetu Tanzania wataiona klabu maarufu ya Sevilla,” alisema.

Sevilla maarufu kama Nervionenses, watacheza na timu moja washirika wa SportPesa kati ya Simba au Yanga Mei 23 mwaka huu, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa, Tarimba Abbas, alisema wanafanya kazi na baadhi ya taasisi kubwa za soka duniani, hivyo kuna umuhimu wa kuleta nchini uzoefu wao.

“Ushirikiano huu unatufanya tuone umuhimu wa kuleta uzoefu wao nchini ili kuwapa nafasi Watanzania kuifurahia Sevilla ambayo ni moja ya timu kubwa Ulaya,” alisema Tarimba.

Sevilla inakuwa timu ya pili kuletwa nchini na SportPesa baada ya Everton ya England iliyokuja miaka miwili iliyopita.

Mabingwa hawa mara moja wa La Liga, wanarudi Afrika kabla hata ya kumaliza mwaka tangu kucheza Spanish Supercup jijini Tangiers, Morocco.

Aidha, walicheza Morocco miaka minne iliyopita dhidi ya Hassania Union Sport d’Agadir.

Naye Katibu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, alisema si jambo dogo kupata ugeni wa Sevilla ambayo inashiriki ligi bora.

“Sevilla ina wachezaji 11 wanaocheza timu za taifa kutoka nchi mbalimbali ikiwamo Argentina, Hispania na Italia, hivyo kama TFF tunaahidi kushirikiana na SportPesa kuhakikisha maandalizi yote yanakwenda vizuri kuelekea mchezo huo,” alisema Kidao.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*