Samatta: Ubingwa muhimu kuliko kiatu cha dhahabu

EZEKIEL TENDWA

NAHODHA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayekipiga na timu ya Genk ambayo juzi usiku ilitwaa ubingwa Ligi Kuu ya Ubelgiji, amesema ushindi huo ni muhimu kuliko kiatu cha dhahabu.

Samatta mwenye mabao 23 anawania kiatu cha dhahabu na Hamdi Harbaoui raia wa Tunisia anayeichezea Zulte Waregem, ambaye amemzidi mabao mawili.

Hata hivyo, Samatta anaweza akampiku Harbaoui katika mchezo wa mwisho kesho dhidi ya Standard Liege kwa sababu mshambuliaji huyo raia wa Tunisia, atakosa mchezo wao wa mwisho kutokana na adhabu anayotumikia.

“Sijali sana kuhusu kiatu cha dhahabu kwa sababu tayari ninacho nilichokihitaji, ubingwa huu ni muhimu sana kwangu kuliko kiatu cha dhahabu,” alisema Samatta.

Genk ilitwaa ubingwa wa nne Ligi Kuu Ubelgiji juzi usiku licha ya kutoka sare ya bao 1-1 na Sporting Anderlencht na hii ni baada ya wapinzani wao wa karibu Club Brugge kufungwa mabao 2-0 na Standard Liege.

Ubingwa huo unamfanya Samatta kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na huenda sasa akakutana na timu vigogo kama vile Barcelona, Juventus, Real Madrid, Manchester City, Liverpool, PSG na Bayern Munich.

Samatta alinunuliwa na Genk mwaka 2016 akitoka kuipa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambayo nayo ilimnunua kutoka Simba.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*