Okwi: Ubingwa Jumanne

SAADA SALIM

MSHAMBULIAJI wa Simba, Emmanuel Okwi, amesema kwa sasa wanapambana kuhakikisha wanashinda michezo yao miwili ukiwamo wa Jumanne inayokuja dhidi ya Singida United ambao utawafanya kutangaza ubingwa moja kwa moja.

Simba wamebakiwa na michezo minne mkononi, lakini wanahitaji pointi tano ili kutangaza ubingwa, hivyo ushindi dhidi ya Ndanda katika mchezo wa kesho na ule wa Jumanne utawafanya wawe wamekusanya jumla ya pointi 91 ambazo haziwezi kufikiwa na wapinzani wao Yanga wenye pointi 83.

Kwa sasa Simba wapo kileleni wakiwa na pointi 85, huku wakitarajiwa kuongeza nyingine kama watashinda dhidi ya Ndanda kesho kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam na kwenda Namfua, mjini Singida kuvaana na Singida United.

Akizungumza na BINGWA jana, Okwi alisema mechi yao dhidi ya Mtibwa Sugar walipambana sana kuhakikisha wanashinda hasa baada ya kupata matokeo mabaya dhidi ya Kagera Sugar na Azam FC, hivyo sasa wanataka kupata ushindi mwingine katika michezo iliyobakia.

Alisema mikakati yao ni kushinda michezo miwili kwanza ambayo itawafanya kutangaza ubingwa ili hata wakicheza michezo mingine wawe hawana wasiwasi wowote.

 “Tunafurahi kupata pointi katika mchezo wetu na Mtibwa Sugar, lakini bado mapambano yanaendelea, kwani tunahitaji kupata pointi tano ambazo zitatufanya tutangaze ubingwa, lakini kwetu tunahitaji kushinda mechi zote tulizokuwa nazo,” alisema Okwi.

Okwi alisema wanahitaji kufanya vizuri zaidi katika michezo hiyo miwili kabla ya kucheza mechi yao ya kirafiki dhidi ya Sevilla ya nchini Hispania, Alhamisi inayokuja Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar, Simba walishinda mabao 3-0, Okwi na John Bocco kila mmoja akifunga bao moja na kufikisha mabao 15, huku la tatu likifungwa na Cletous Chama.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*