Nini kimemkumba Coutinho Barcelona?

CATALONIA, Hispania

KUNA vitu vingi ambavyo Philippe Coutinho alivitegemea na vingine hakutaka vimtokee ndani ya Jiji la Catalonia ambako timu yake ya Barcelona inapatikana.

Moja ya jambo ambalo hakupenda alishuhudie ni kusherehekea mwaka mmoja tangu awe mchezaji wa Barcelona akiwa benchi, wakati timu yake hiyo ikichuana na Getafe wikiendi iliyopita.

Januari 6 mwaka jana ndio ilikuwa siku ya Coutinho kutambulishwa kama mchezaji wa Barca akitokea Liverpool, lakini Januari 6 mwaka huu, alianzia benchi dhidi ya Getafe.

Ni kitu ambacho hakutaka kitokee kabisa, kwani ilikuwa ni siku yake maalumu ya kuonesha soka safi akiwa anatimiza mwaka mmoja tangu awe mchezaji wa Barcelona.

Kiufupi ni kwamba, Coutinho alianzia benchi kwa mara ya nne mfululizo katika mechi ya La Liga msimu huu.

Kwake yeye, hizo ni mechi nyingi kuanzia benchi kwani msimu uliopita ulikuwa maalumu kwake kuzoea mazingira ya Hispania, hivyo ilitegemewa kwamba msimu huu ulikuwa ni wa uhakika kuanza.

Hii inaweza kuwa ni taarifa njema mno kwa mashabiki wa mahasimu wakubwa wa Barca ambao ni Real Madrid na Espanyol na hata wale wa Liverpool.

Lakini, kwa wengine watasikitika kushuhudia nyota huyo akipata shinda ya kuanza kikosi cha kwanza. Cha kujiuliza kwa sasa ni jambo gani lililomkumba mchezaji huyo aliyeweka rekodi ya usajili wa bei mbaya.

Ishu ilianzia hapa

Katika majira ya kiangazi mwaka 2017 baada ya Barcelona kumpoteza Neymar, wababe hao walianza kumfukuzia Coutinho lakini ghafla wakahamia kwa Ousmane Dembele na kumsajili winga huyo wa Kifaransa kutoka Borussia Dortmund.

Barca walidai kwamba mpango huo wa kumsajili Coutinho ulikuwa ni wa muda mrefu, kwani waliamini angeweza kuwa mrithi wa kiungo wao wa zamani, Andrés Iniesta.

Hivyo usajili wa Dembélé ulilenga kuziba pengo la Neymar.

Ikumbukwe katika kipindi hicho, Liverpool waligoma kumwachia Coutinho na kumnyima fursa ya kuhamia kwenye timu aliyoota kuichezea tangu akiwa mdogo.

Usajili wa Dembele nao haukutoa matunda mapema kutokana na jeraha la msuli wa paja lililomkumba.

Changamoto

Kutokana na kuumia kwa Dembele, Barca waliingia kwenye wakati mgumu wa kuchezesha timu iliyo na idadi ndogo sana ya wachezaji mahiri.

Kuna wakati kocha, Ernesto Valverde alitumia muundo wa 4-3-3 lakini Barca ilishindwa kuonesha kiwango cha kueleweka na hakukuwa na maelewano katika mfumo wa kiuchezaji.

Valverde aliibuka na mbinu nyingine ya kupunguza matatizo ya kiulinzi kwa kutomtumia Lionel Messi kama winga na kuanza kutumia muundo wa 4-4-1-1.

Timu ilianza kuonesha utulivu. Messi alirudi kwenye kiwango chake, viwango vya Sergio Busquets, Ivan Rakitic na kipa Marc-André Ter Stegen pia vikaifanya Barca iwe timu tishio zaidi.

Mrithi amepatikana

Ilipofika Januari, 2018, Barca ikarudi tena kumsajili Coutinho huku kiwango chao kiujumla kikiwa bora, hivyo ikadhihirika kwamba mrithi wa Iniesta amepatikana katika wakati sahihi.

Mwanzoni alianza kutumika kama kiungo wa kati kwenye mfumo wa 4-3-3. Kiufupi halikuwa chaguo sahihi kiulinzi hivyo ukarudishwa muundo wa 4-4-1-1, Coutinho akitumika upande wa kushoto.

Majukumu aliyokuwa nayo ni kucheza kama kiungo wa kati, winga na kiungo wa kushambulia, kwa kiasi kikubwa muundo huo ulimfaa Coutinho na ndipo alipoanza kuisaidia timu yake katika ufungaji mabao.

Nini kimebadilika msimu huu?

Valverde aliamua kurudi kwenye utamaduni wa Barca kutumia muundo wa 4-3-3 kwa sababu tayari alikuwa na kikosi kilichosheheni wachezaji mahiri, hasa baada ya kuongezeka kwa winga, Malcom.

Hiyo ilimaanisha Coutinho angetumika tena kama kiungo wa kati, lakini katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, timu yake ya taifa ya Brazil ikagundua iwapo atatumika hivyo ni lazima atakuwa mzigo katika kutimiza majukumu ya ulinzi.

Aidha, muundo huo wa 4-3-3 ulimrudisha Messi winga ya kulia lakini hakukaa upande huo muda mwingi kwa sababu alitakiwa kucheza pia kama namba 10. Hilo likaufanya upande wa kulia kubaki wazi muda mwingi.

Timu pinzani zikatumia upenyo huo kuishambulia Barca. Valverde akatumia mbinu ya kumsogeza Rakitic upande wa kulia kuziba pengo la Messi (na hasa wakati ambao beki, Sergi Roberto alipokuwa akishambulia zaidi).

Jambo la hatari zaidi ni kwamba, safu ya ulinzi nayo ikawa inabaki wazi muda mwingi, ikimwachia majukumu yote ya ulinzi kiungo mkabaji, Busquets.

Ukiunganisha vitu hivyo viwili, unagundua kwamba Barca ilikuwa na matatizo makubwa ya kiulinzi msimu huu na mara kwa mara ilijikuta ikishindwa kupata ushindi na hata kupoteza kwenye mechi za La Liga.

Sababu kuu ni hii

Valverde akarudi tena kwenye muundo wake wa 4-4-1-1, ikiwa na maana Coutinho angerudishwa upande wa kushoto licha ya kwamba katika mazoezi ya kujiandaa na msimu huu alinolewa kucheza katikati.

Mabadiliko hayo ya muundo na mfumo wa kiuchezaji ndiyo yaliyosababisha Coutinho kutoonesha kiwango cha kuridhisha msimu huu licha ya kwamba ameweza kufunga mabao katika baadhi ya mechi kubwa.

Baada ya hapo aliumia na kukosa baadhi ya mechi na katika kipindi hicho Dembele alianza kuonesha kiwango safi kiasi cha kujihakikishia nafasi kwenye timu ambayo ilitumia muundo wa 4-4-1-1, tofauti na ule wa 4-3-3 ambao yeye na Coutinho wangeweza kuanza.

Ni muundo na mfumo wa kiuchezaji katika timu ya Barca sambamba na kiwango cha Dembele, vinavyosababisha Coutinho ashindwe kupata nafasi.

Suala hilo linamfanya Coutinho aombe aidha Dembélé ashuke kiwango au Luis Suárez aumie, ili Valverde aanze kumtumia kwenye muundo wa 4-3-3 kwa mara nyingine tena.

Si kwamba amesahau kabisa kucheza soka, ni kwamba Valverde amekosa mbinu za kutosha za kiufundi kwa ajili ya kumwinua Coutinho aliyeanguka.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*