Ni jukumu la kila mmoja kuwa hivi kwa mwenzake


UKWELI ni kwamba mapenzi ni suala linalohitaji kila mmoja ajitoe kwa mwenzake ili ile raha na amani inayotamaniwa na kila mmoja iweze kupatikana.

Ukiwa katika mahusiano suala la kujiangalia wewe tu inabidi lisiwepo ikiwa unahitaji furaha na amani.

Sasa baada ya kuamua kuingia katika maisha ya ndoa zile habari za safari zisizoeleweka zinabidi zisiwepo tena.

Yale mambo ya kufanya huku ukijiangalia wewe tu pia ni lazima yaishe ikiwa unataka mahusiano yako yaendelee kuwa na amani na utulivu.

Ile dakika ya kwanza ulipokubali kuwa naye, ujue uliamua kutoa neno mimi na ukaweka sisi. Uliamua kutoa neno vya kwangu na kuweka vya kwetu.

Wewe si yule tena ambaye utaaamua kurudi nyumbani muda unaotaka. Wewe si yule tena ambaye unaweza kuamua kuvaa chochote ama kuongea na yeyote katika mazingira yoyote.

Wewe si yule tena unayeweza kubadilika badilika unavyojisikia na usiulizwe maswali mengi.

 Japo mwili ni na nafsi ni vyako ila kuna mtu anakuhusu sana kiasi cha kufanya muonekane mwili mmoja.

Hautakiwi kujifikiria mwenyewe mfikirie na mwenzako. Ukiwa na furaha basi inabidi na yeye imhusu hata kidogo.

Akiwa na huzuni inabidi ufanye apate raha na vicheko. Hayo ndiyo mapenzi na hivyo ndivyo wapendanavyo kiuhalisia wanavyoishi.

 Hapa ukiamua kujiangalia tu wewe na kumsahau mwenzako ujue utakuwa umeingiza ugonjwa katika mahusiano yenu.

Eti unamwona ana huzuni badala ya kutaka kujua chanzo unamuuliza tu honey mambo vipi, japo anakujibu kiunyonge wewe hujali.

Ni lazima mwenzako atakufikiria vingine ingawa si wewe uliyemfanya kuwa na huzuni. Unampigia simu mpenzi wako mara ngapi?

 Nimewahi kuwasikia baadhi ya wasichana, dah! Mwanaume yule hata hanipendi, tokea asubuhi kanipigia simu mara mbili tu.

Unadhani ni nani mwenye jukumu la kumpigia mwezake? Haya ni matokeo ya kujifikiria sana mwenyewe. Ni matokeo ya ubinafsi ambayo baadaye huja kuzorotesha hali ya furaha katika uhusiano husika.

Watu wengi huendekeza ubinafsi na ndiyo maana wanataka wao tu kuoneshwa wanapendwa na kujaliwa. Kila muda wanataka wao tu ndiyo waanze kuulizwa kama wamekula au wameshinda vizuri. Wao kimya!

Hivi unadhani ni nani hasa mwenye jukumu la kumpenda mwenzake? Ulipoamua kuwa na huyu uliye naye basi kuanzia pale haukutakiwa kuanza tena kujifikiria wewe. Mapenzi ni upamoja.

Tendo unalotaka kufanyiwa wewe basi mfanyie na mwenzako. Hakuna anayechukia kupigiwa simu na mpenzi wake wa dhati. Hakuna anayependa yeye tu ndiyo akutafute.

Ukijiangalia tu wewe unaharibu mapenzi. Katika hili la kujiangalia tu pekee ndiyo maana wanawake wengi hudhani jukumu la kusaidia kwenye tatizo liko kwa wanaume tu.

Hata wenzao wanapopatwa na matatizo wao kimya. Ila wao wanapopatwa na matatizo utasikia wakiambiwa wewe si una mwanaume! Mwambie akusaidie sasa, huo ndiyo umuhimu wa kuwa na mwanaume!

Ukiacha kuutoa ubinafsi katika mahusiano yako kila siku mwenzako atajikuta akikereka na matendo yako. Maana ukiwa nao hata kushikwa shikwa unaweza kuona si hatari, si mwili wako bana.

Kila mmoja na mwili wake sasa kwani kushikwa shikwa ndio nini! Hapo ujue umeshindwa kumfanya mwenzako kuwa wewe.

Kila kinachohusu wewe na maisha yako inabidi mwenzako ashiriki aidha kwa kukubali, kukataa ama kutoa maoni.

Mwenzako akiwa na mamlaka hayo ujue hapo mahusiano yanaweza kuwa na amani na ubora unaohitajika.

 Ila si kila kitu kizuri unataka ufanyiwe wewe tu wakati wewe unajifanyia ya kwako unavyojisikia. Kupendana ni pamoja na kila mmoja kujihisi ana mamlaka na mwenzake.

 Huwezi kusema unampenda sana ikiwa kila jambo jema unataka ufanyiwe wewe tu. Sasa unampeda kivipi?

Mapenzi hayaishi mdomoni, matendo yako mazuri ndiyo kipimo cha upendo wako kwake. Acha kujifikiria wewe tu, mfikirie mwezako ili kila mmoja aone fahari ya kuwa na mwenzake. Ubinafsi unaua mapenzi.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*