‘NEYMAR’ Haeleweki duniani, haeleweki mbinguni

NA AYOUB HINJO

KADIRI siku zinavyosogea kupisha jua kuchomoza na kuzama kisha mwezi kuchukua nafasi yake kumulika anga wakati wa kiza kinene, kuna mambo mengi hutokea katika uso wa dunia hii tunayoishi ndani yake.

Ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kila siku ambayo yamekuwa hayaeleweki kwa baadhi ya watu huku kwa wengine yakionekana kwenda sawa kama kupiga mstari mnyoofu na rula ya mita 30.

Wakati mwingine ni ngumu sana kuyaelewa maisha, si rahisi hata kidogo japokuwa tunaishi ndani ya ulimwengu huu uliojaa shida, mateso, raha na karaha kwa muda wote.

Kwa ukaribu zaidi, itazame sura ya Neymar, inawezekana kuna mengi yanakufikirisha kadiri unavyoitazama au kuikumbuka taswira yake ilivyo.

Inawezekana pia dunia tunayoishi sisi, si ile anayoishi Neymar, achana na mambo mengine yanayomzunguka nje ya uwanja.

Mtazame Neymar aliyeanza safari ya soka miaka mingi kidogo nyuma akiwa Santos FC ya nchini Brazil, aliishi ndani ya pepo yake iliyojaa matumaini makubwa ya Wabrazil kuwa shujaa mpya amezaliwa.

Habari za ubora na uwezo wa Neymar zilipenya kwa kila mmoja duniani japo kwa wakati huo alikuwa akifanya yake nchini Brazil.

Wapo waliowahi kusema kipaji hakijifichi, pamoja na hayo yote, Neymar, alisubiriwa Ulaya. Sehemu ambayo inaaminika mwanasoka atakumbana na mambo mengi hasa ushindani.

Muda ulipofika, kila mmoja alimwona Neymar akiwa Barcelona, ujio wake uliifanya klabu hiyo kutengeneza kombinesheni ya wachezaji watatu hatari katika idara ya ushambuliaji MSN (Messi, Suarez na Neymar).

Lakini mwisho wa siku Neymar alikimbia Barcelona, hakuhitaji kuwa chini ya kivuli cha mchezaji mwingine, alitamani kuishi sehemu ambayo atatajwa kuwa mfalme.

Aliondoka na kujiunga na PSG tena kwa uhamisho wa mchezaji ghali zaidi duniani, mambo yalianza kubadilika ndani ya klabu hiyo.

Wote walioonekana wafalme ilibidi waisikilize sauti ya Neymar inahitaji au inataka nini, si wachezaji tu hata kocha ambaye alikuwepo alimsikiliza zaidi nyota huyo.

Siku tatu zilizopita, Neymar alitimiza miaka 27, inashtua kidogo, ni wakati ambao wachezaji wengi wanaishi kwenye kilele cha ubora wao katika soka.

Ni muda huo ambao Neymar ameanza kupunga mkono wa kwa heri, unajua kwanini? Nitakueleza huko mbele jinsi vinasaba vya soka vinavyojaribu kupita mbali ya staa huyo.

Katika umri wake bora kabisa kisoka, Neymar yuko PSG akicheza michezo ya kitoto na akina Kylian Mbappe, sidhani kama tunatakiwa kusubiri zaidi ya kukubaliana kuwa staa huyo ni Theo Walcott wa bei ghali.

Rudi miaka kadhaa nyuma, Neymar alikuwa mmoja wa nyota ambao walitazamiwa kushindana bega kwa bega na Cristiano Ronaldo au Lionel Messi.

Moja, Neymar ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa mno hasa pale anapoamua kucheza mpira, binafsi naamini mpaka sasa dunia imeona mambo machache sana kutoka kwake.

Mbili, hakuuheshimu muda, jaribu kuitazama Barcelona hii ya sasa kama Neymar angekuwepo ndani yake, taratibu alikuwa anachukua ufalme wa Messi.

Tangu aingie barani Ulaya hakuna Neymar bora zaidi ya yule aliyewahi kuvaa jezi ya Barcelona, licha ya kuwa chini ya Messi bado aliweza kufanya mambo makubwa na kwa kiasi fulani alitengeneza pepo yake kando ya staa huyo wa Argentina.

Mchezaji wa kariba ya Neymar, ana uwezo wa kufanya kitu ambacho hujawahi kukiona kokote kule. Kitu ambacho hujawahi kukipatia picha.

Aina ya mabao aliyokuwa akifunga ni yale ambayo hata wataalamu wa kutengeneza filamu za michezo waliwaza na kujaribu kutengeneza filamu ya shujaa wa soka aliye kwenye maisha ya uhalisia.

Huyo ndiye Neymar. Mchezaji anayefanya maajabu kwenye maisha ya kweli.

Ilikuwa ni ngumu kutabiri atakachokifanya sekunde tatu baadaye akiwa na mpira mguuni mwake lakini tayari unakuwa umeshajua kuna kitu cha ajabu kitatokea.

Angeweza kukokota mpira kwa kasi ya roketi na kuwapita wachezaji wanne au watano, akichanganya miguu kwa chenga za gemu la Fifa. Rahisi kihivyo tu.

Angeweza kufunga bao la dakika za mwisho kwa mguu wowote na mpira ungeenda kutua nyavu za juu, pembeni kabisa. Kwisha kazi.

Angeweza kufunga bao kali la mpira wa adhabu kutoka umbali wa yadi 40. Kwenye pembe ngumu mno.

Alibarikiwa kila kitu, lakini mpaka kufikia sasa akiwa na miaka 27 bado hajui anahitaji kitu gani, sahau kuhusu pesa anazozipata kutokana na utanashati wake.

Weka kando wasichana wanaogongana katika gheto lake kila kukicha, kwa umri wake alistahili kuwa mmoja wa wachezaji walioiweka dunia chini ya nyayo zake.

Inaaminika umri huo unakuwa tayari umepitia mambo mengi, vishawishi na starehe nyingi. Kwa kifupi, kuna kuwa hakuna kipya ndani yake.

Nyota wengi waliotamba kwa vipindi katika soka, walikuwa kwenye umri wa aina hiyo, kumbuka akina Ricardo Kaka, Robin van Persie na wengine wengi kwa wakati tofauti.

Bado tunaendelea kumtazama Neymar, haeleweki yupo katika kundi gani, bado hatazamiki kama zamani.

Katika fainali za Kombe la Dunia mwaka jana nchini Urusi, kila shabiki wa soka alionekana kuwa kinyume na Neymar, hakufanya kile alichotegemewa na wengi, alikatisha tamaa na kuvunja mioyo ya waliokuwa na imani naye.

Neymar hana utofauti na Luis Nani ambaye alitabiriwa kufanya makubwa kando ya Ronaldo wakati wapo Manchester United hata alipoondoka kwenda Real Madrid.

Nani alishindwa kujazia mchanga shimo lililoachwa na Ronaldo, mwisho wa siku licha ya kipaji chake kikubwa alionekana mchezaji wa kawaida kuwahi kutokea Manchester United.

Si rahisi kihivyo kuishi kwenye ndoto za wengi ingawa bado ni rahisi kutimiza kile kinachotazamiwa na wengi kama kutakuwa na juhudi kubwa kwa mtu husika.

Sioni mwendelezo wa Neymar bora zaidi, bado haeleweki duniani wala mbinguni. Tayari amevunja mioyo ya wengi, tatizo ni kwamba jamaa hayupo ‘siriaz’ sana.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*