Ndayiragije ataja sababu za Kaseja kutokea benchi

MWAMVITA MTANDA NA TIMA SIKILO

KOCHA mkuu wa timu ya KMC, Mrundi Etienne Ndayiragije, amesema sababu ya mlinda mlango namba moja wa timu hiyo, Juma Kaseja, kutokea benchi ni pamoja na kumpa nafasi Jonathan Nahima ambaye bado ni chipukizi.

Katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Yanga, kipa huyo mkongwe alitokea benchi hali iliyoshangaza mashabiki wa soka wakiamini kuwa pengine ameanza kushuka kiwango.

KMC ilifungwa na Yanga mabao 2-1, bao la kwanza lilifungwa na Papy Kabamba Tshishimbi na la pili mchezaji wao, Ally Ally, alijifunga baada ya Nahodha Ibrahim Ajib kupiga krosi. KMC walipata bao kupitia kwa Mohamed Rashid.

Akizungumza na BINGWA jana, Ndayiragije, alisema kutokana na uzoefu wake katika soka anatambua kwa haraka  kipaji cha mchezaji, ndio maana ameanza kumwamini kipa huyo na kumpa  nafasi ya kwanza katika mchezo huo.

“Ukizungumza Kaseja ni mchezaji wa levo nyingine kabisa, hauwezi hata kidogo kumfananisha na Jonathan, lakini nimeanza kumpa nafasi ili nisitegemee  kipa mmoja, nina imani ameonesha uwezo wake na hilo halina tatizo kwa Kaseja sababu naye anatamani kumwona akifanya vizuri zaidi,” alisema Ndayiragije.

Aidha, kocha huyo alisema mikakati  yake ni kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi ndani ya kikosi hicho lakini itatokana na juhudi zake.

“Mara nyingi napenda kuongea nao wanasikiliza kile ninachowaambia, lakini nataka wapate nafasi wote lengo ni kuisaidia timu, hivyo usishangae ukaona  nawatumia ambao huwa hawapati nafasi za kwanza lengo ni kuwapa uzoefu,” alisema Ndayiragije.

Katika hatua nyingine, Ndayiragije, amesema hamtumii mshambuliaji wake, Elius Maguli, kwenye kikosi chake cha kwanza kutokana na kushuka kwa kiwango chake.

Michezo kadhaa imepita Ndiyiragije hajamtumia Maguli wala kumpanga katika wachezaji wa akiba.

Kocha huyo alisema si Maguli tu ambaye hamtumii, ni wachezaji wengi lakini kila mchezaji ana sababu zake.

Alisema Maguli yupo na wakati wowote anaweza kupata nafasi ya kucheza, atakapokuwa vizuri atarudi katika nafasi yake.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*