Msimu wa pili ‘MultiChoice Talent Factory’ wazinduliwa

NA MWANDISHI WETU

VIJANA 60 kutoka barani Afrika ikiwemo Tanzania, watapata fursa ya udhamini wa kujifunza uzalishaji wa filamu na vipindi vya runinga kwa mwaka mzima utakaoendeshwa katika vituo vitatu vya Nairobi, Lusaka na Lagos kwenye msimu wa pili wa MultiChoice Talent Factory kuanzia juzi mpaka Julai 14, mwaka huu.

Akizungumzia fursa hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, Jacqueline Woiso, alisema kwa upande wa Tanzania, kuna nafasi nne za udhamini ambao wanafunzi hao wataungana na wenzao kutoka Kenya, Uganda na Ethiopia katika kituo cha mafunzo cha Nairobi, ambapo watafundishwa na wakufunzi mahiri wenye ujuzi mkubwa.

“Programu hii ilizinduliwa rasmi Mei 2018 kwa lengo la kuwanoa vijana wa Kiafrika katika tasnia ya filamu ili kuwapa upeo, uwezo, ujuzi na weledi wa kiwango cha kimataifa katika uzalishaji na biashara ya filamu kwa ujumla.

“Kwa wanaotaka kushiriki watembelee www.multichoicetalentfactory.com na kisha kufuata maelekezo ya namna ya kujisajili na endapo watapata tatizo lolote, wanaweza kutuma e-mail info@multichoicetalentfactory.com au kupiga simu+255 756 753 201 kwa maelekezo zaidi,” alisema Woiso.

Woiso alisema kama sehemu ya programu, watengenezaji filamu wadogo watapatiwa mafunzo na uzoefu wa vitendo katika tasnia ya filamu kwa kuzingatia simulizi za visa, uzalishaji, sauti na kuongoza ikiwemo na maeneo mengine muhimu.

“Vituo hivi pia vinatoa fursa kwa wanafunzi kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa sekta hiyo, kufanya kazi za kuzalisha vipindi vya runinga, maigizo na kuandaa maudhui asilia ambayo yatakuwa yakirushwa hewani kwa njia mbalimbali ndani ya M-Net kwa kupitia DStv,” alisema.

Aliongeza: “Darasa la kwanza la programu hii  litakamilika Oktoba mwaka huu na tayari limeonyesha mafanikio makubwa, ambapo wanafunzi wameshiriki katika kazi mbalimbali ikiwemo utengenezaji wa vipindi halisia vya muziki kama Coke Studio, Pambio, Turn-Up na Telenovela ya Kiswahili maarufu Selina.

“Nawasihi vijana wetu wa Tanzania wenye ari na nia ya kuwa nyota wa uzalishaji wa filamu duniani, kuhakikisha hawakosi nafasi hii. Wajiandikishe ili waweze kupata fursa hii muhimu,” alisema Woiso.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*