Mipango, hesabu vitaibeba Simba leo


NA ZAINAB IDDY      

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye  michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Simba, leo watashuka dimbani kutupa karata yao ya mwisho katika hatua ya makundi.

Wekundu wa Msimbazi watahitimisha mchezo wao wa Kundi D wakiikaribisha AS Vita Club kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo ya ushindi katika mchezo wa leo ni muhimu zaidi kwa Simba na Taifa kwa ujumla, kwani mafanikio yoyote ambayo yatapatikana yataibeba Tanzania.

Hakuna ubishi kwamba mchezo wa leo ni mgumu kwa Simba, kutokana na kila timu iliyopo katika Kundi D kuwa na nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali kulingana na hesabu zilivyo iwapo itashinda.

Ukiangalia msimamo wa Kundi D ulivyo na pointi zao, ni wazi kwamba kila timu imepania kupata matokeo ya ushindi, iwe inacheza uwanja wa nyumbani au ugenini, kwa sababu zote zinaweza kusonga mbele.

Tangu kuanza kwa hatua ya makundi, mechi za ugenini zinaonekana kuwa ngumu kwa wageni, hata ukiangalia matokeo ya nyuma Al Ahly ndio waliweza kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya wenyeji wao, JS Saoura.

Pia Waalgeria hao waliweza kufurukuta ugenini nchini DRC na kulazimisha sare ya mabao 2-2, hii ikimaanisha ushindani ni mkubwa na hesabu ni ngumu.

Kwa uhalisia, AS Vita si timu nyepesi, maana tumeona namna ilivyowapa tabu Al Ahly wakicheza nyumbani kwao, lakini pia ikumbukwe Simba walichapwa mabao 5-0 kule DRC.

Ukifuatilia kwa umakini mechi walizocheza AS Vita utagundua kwamba Simba wanakutana na timu ngumu yenye uchu wa kusonga mbele katika michuano hii.

Kuna msemo wa Wahenga unaosema ‘jitihada hushinda kudra’, hivyo kama Simba wakicheza kwa malengo, nia na kuweka hesabu zao sawa, basi upo uwezekano wa kupenya hatua ya robo fainali.

Ili kufanikisha hili, ni lazima wachezaji na benchi la ufundi wajipange kukubali mkakati uliopo katika Kundi D kwamba hakuna timu iliyokubali kufungwa nyumbani.

Wachezaji wanapaswa kucheza kwa ushirikiano na kila mmoja anatakiwa kutumia nguvu, akili na juhudi binafsi ili kutimiza majukumu yake kikamilifu.

Kama hili litazingatiwa, itawasaidia Simba kupata matokeo chanya kwenye uwanja wa nyumbani na kuwapa furaha mashabiki wao ambao wanaiombea timu yao ipige hatua zaidi kimataifa.

Ushindi wa aina yoyote utakuwa na manufaa kwa Simba, kwani utawawezesha kutinga hatua inayofuata ya robo fainali ambayo kila shabiki na mwanachana wa klabu hiyo anaitamani.

Wachezaji wote ambao watapata nafasi ya kucheza dhidi ya AS Vita ni vyema wakafahamu kuwa wanatazamwa na Watanzania walio wengi kwa sababu wamebeba furaha yao, hivyo wajitahidi kupambana na kufanya kazi sawa sawa.

Pia ni vizuri benchi la ufundi liachwe lifanye kazi yake kikamilifu, yaani kusiwepo viongozi wanaoingilia majukumu yao.

Ninaamini kila kitu kinawezekana chini ya jua, kama Simba iliwahi kuvunja rekodi na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2013, kwanini safari hii washindwe kufanya hivyo.

Hakika itakuwa jambo la ajabu na aibu kama suala la kukata tamaa litapewa kipaumbele hivi sasa, wakati wachezaji wana uwezo wa kupindua meza kibabe na kuwashangaza wapinzani wao.

Licha ya tofauti zilizopo, lakini mashabiki  wana jukumu la kuwapa sapoti Simba, ambao wanaiwakilisha nchi katika michuano hii mikubwa barani Afrika.

Hakuna ubishi mashabiki ni muhimu katika kusaidia ushindi wa Simba, ambao utawatoa kimasomaso Watanzania, ikumbukwe kwenye mchezo mgumu uliopita dhidi ya Al Ahly, nguvu yao ilihusika kuleta matokeo chanya.

Hakika ushangiliaji utawafanya wachezaji watambue kuwa wana kazi kubwa ya kufanya uwanjani, hivyo watajitahidi kupambana kwa nguvu zote ndani ya dakika 90 za mchezo.

Kila la kheri Simba, fanyeni kazi kwa manufaa ya Taifa lenu ili mchukue pointi muhimu ambazo zitaweka historia mpya na kuipa klabu mafanikio.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*