Masawe: Tutalipa kisasi kwa Mwadui

NA DAMIAN MASYENENE, MWANZA

NAHODHA wa Stand United, Jacob Masawe, amejipanga vilivyo kwa lengo la kulipa kisasi dhidi ya Mwadui katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, mkoani hapa.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza, Stand United walikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mwadui uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga.

Akizungumza na BINGWA mkoani hapa juzi, Masawe alisema wanaendelea na mazoezi makali chini ya kocha wao, Athuman Bilal, ili kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya wapinzani wao.

Masawe alisema wameupa umuhimu mkubwa kushinda mchezo huo kutokana na kushika nafasi ya 17 ambayo ni mbaya katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Alisema wanahitaji kushinda ili waweze kujiongezea pointi ambazo zitawawezesha kusogea katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo.

“Tunaendelea na maandalizi, mwalimu anazidi kutupatia mbinu na vitu vizuri, tumeupa kipaumbele mchezo huu kuhakikisha tunapata ushindi kwa sababu hatuko kwenye nafasi nzuri.

Tuna uwezo wa kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wao,” alisema Masawe.

Kwa upande wake, Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu, alisema anafahamu wapinzani wao na wataingia uwanjani kwa nguvu kubwa ili wasipoteze mchezo huo.

“Mechi ya Stand United ni kubwa tunafahamu wako sehemu mbaya, watakuja kwa kujihami sana na kutumia nguvu nyingi.

Sisi kama timu lazima tukabiliane na hali hiyo, tumejiandaa ili tubaki na pointi nyumbani kwa sababu hatujawahi kupoteza mchezo hapa nyumbani,” alisema.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*