Man Utd yajiharibia yenyewe ‘top four’


MERSEYSIDE, England

TANGU Man Utd imwajiri kocha, Sir Alex Ferguson mwaka 1986, klabu hiyo ilikuwa haijawahi kupoteza mechi tano mfululizo za ugenini katika michuano yote ndani ya msimu mmoja.

Lakini, kichapo cha mabao 4-0 walichokipata jana dhidi ya Everton kilikamilisha mechi tano mfululizo walizopoteza wakiwa katika uwanja wa ugenini, wakifungwa pia na Arsenal, Wolves (2) na Barcelona.

Kikosi hicho cha kocha Ole Gunnar Solskjaer ambacho katika siku chache zilizopita kilielezewa na kocha wao wa zamani, Louis van Gaal kuwa bado ‘kinapaki basi’ kama ilivyokuwa enzi za Jose Mourinho.

Hata hivyo, safari hii Van Gaal aliongeza si tu kwamba United inajilinda zaidi, pia inapaki basi hata mbele ya mlinda mlango wao, David de Gea, ambaye katika mchezo huo wa jana alikutana na wakati mgumu.

Kichapo hicho cha mabao mengi zaidi tangu Solskjaer apewe kibarua cha muda hadi kusaini mkataba wa miaka mitatu, kimekuja katika mwendelezo wa matokeo mabovu yaliyoanza kurudisha kumbukumbu za nyuma.

Ikiwa katika nafasi ya sita kwa sasa, United ilijikuta ikiwa nyuma kwa bao zuri la straika, Richarlison, ndani ya dakika 13 tu tangu mchezo huo uanze, baada kuunganisha pasi ya kichwa iliyopigwa na Dominic Calvert-Lewin.

Everton hawakuonesha kuridhika na bao hilo, waliendelea kulishambulia lango la United huku wageni wao hao nao wakifanya jitihada za kulisawazisha bila mafanikio.

Dakika ya 28, Gyfli Sigurdsson aliwainua mashabiki wa Everton kwa kufunga bao la umbali mrefu baada ya kufanya shambulizi la kushtukiza lililopitia kwa kiungo, Idrissa Gana Gueye na kufanya matokeo kuwa 2-0 hadi mapumziko.

Mabao mengine makali yaliyofungwa na Luca Digne aliyefyatua shuti kali nje ya 18 baada ya kona iliyochongwa na Sigurdsson kuokolewa na De Gea, kabla ya Theo Walcott kupigilia msumari wa mwisho kwenye jeneza la United.

Matokeo hayo yanaiacha United kwenye wakati mgumu wa kuhakikisha inashinda mechi zake zilizosalia ili iweze kwenda sawa na kasi ya wapinzani wao; Arsenal, Chelsea na Spurs.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*