googleAds

Kenny Guitar Mkali wa gitaa aliyeupaisha wimbo ‘You Are The Best’ wa Ommy Dimpoz

NA CHRISTOPHER MSEKENA

MIONGONI mwa wimbo unaokonga mioyo ya watu kwa sasa hapa Bongo ni You Are The Best wa mwimbaji, Omary Nyembo ‘Ommy Dimpoz’, iliyonogeshwa kwa gitaa asili ya Hispania na kufanya wimbo huo uwe burudani kwa yeyote anayesikiliza.

BINGWA lilikutana na mpiga gitaa la solo, Kennedy Masanja ‘Kenny Guitar’, ambaye ndiye alipiga chombo hicho kwenye wimbo huo ambao kwa sasa umeshika namba za juu kwenye chati mbalimbali za muziki ndani na nje ya Tanzania ili ufahamu mengi kutoka kwake, karibu.

BINGWA: Kwanini umeamua kujiingiza moja kwa moja kwenye upigaji gitaa na si kuimba kama wanavyofanya vijana wengi?

Kenny Guitar:  Kabla ya hapo nilikuwa ninaimba kawaida na mtu aliyenivutia zaidi kupiga gitaa ni Kigumu kwa sababu anaimba na kupiga gitaa na nilijikuta napenda sana gitaa baada ya kuona uimbaji wangu unahitaji nitoe hela na mimi sina chanzo chochote cha mapato.

Nikaona nikiweza kupiga gitaa nitaajiriwa kwenye bendi, nitalipwa na nitaweza kukidhi mahitaji yangu. Mwaka 2010 nikiwa Morogoro, nikaingia kwenye mambo ya ‘live band’, huko nikakutana na watu wenye uwezo ambao ni Wakongo nikaendelea kujifunza kupitia wao, nikazidi kupanda daraja.

Nikafanya kazi kwenye bendi kama tatu hivi kwa sababu kule wenzetu wana madaraja, kuna bendi kubwa kabisa inaitwa Waluguru Original ambayo huwa inazipokea bendi kama Fm Academia, Malaika Bendi na nyingine zikiwa na shoo kule Morogoro.

Kule nilikwenda kusoma, nyumbani kwetu ni hapa hapa Dar es Salaam. Ilitokea changamoto moja kuwa pale Morogoro sina ushindani, hakuna anayeniweza kwa kupiga gitaa. Ikabidi nitoke kule nirudi Dar na sikutaka kurudi nyumbani nikakaa geto kwa mshkaji huku napambana.

BINGWA: Ilikuwaje ukaanza kufanya kazi na wasanii wa Bongo Fleva kama mpiga gitaa?

Kenny Guitar: Katika kuhangaika nilikuwa na Beka Ibrozama, nilimwambia napiga gitaa, akaniunga kwenye bendi yake nikawa napiga, safari ikaanzia hapo, nikakutana na Walter Chilambo ambaye aliniunganisha na Jux.

Juzi nilipiga naye sana mpaka tukaenda Zanzibar, mpiga ngoma wake ambaye yupo THT, anaitwa Ezze. Baada ya kwenda Zanzibar kurudi alipenda upigaji wangu wa gitaa na kwa kuwa alikuwa anahusika na Fiesta, akaniunganisha nikafanya shoo zote za Fiesta na baada ya kumalizika Fiesta nikaendelea kufanya kazi kwenye bendi kule Zanzibar ambako napiga mpaka sasa hivi.

BINGWA: Kitu gani kilifanya Ommy Dimpoz akuamini kuwa unaweza kupiga gitaa kwenye wimbo wake YoAre The Best?

Kenny Guitar: Nilikutana na Cheed, msanii wa Ali Kiba, aliyeimba Masosy kwenye mtandao, akaniambia niwe naenda Kings Music ili akiniona Kiba chochote kinaweza kutokea.

Nikawa naenda Kings Music na siku Ali Kiba akaniona akakubali upigaji wangu wa gitaa akaniambia nitulie na yeye anataka kuanzisha bendi kwa hiyo nitulie, Cheed sasa ndiyo aliniunganisha na Ommy Dimpoz.

You Are Best ni wimbo uliokuwa unahitaji gitaa na ukisikiliza yale ni mahadhi ya Kizomba, Kizomba baba yake mdogo ni Spanish Guitar na ndani yake kuna Arabic kwa hiyo nikajiongeza pale studio, nikapewa wimbo, watu wakanitazama kwa taswira ya kawaida na mimi nilishazoea mpaka niguse gitaa ndiyo watu wakubali.

Basi ile nimepiga kidogo tu, Ommy Dimpoz, akaniambia nisiongeze inatosha akapenda sana japo mimi nilikuwa nafanya kama ‘free style’ tu. Dimpoz aliumia kuwa nina uwezo mzuri na kwanini bado nahangaika, nikamwambia nimeshafanya kwa watu wengi lakini nafikiri kwako ndiyo wakati sahihi.

BINGWA: Ujuzi ambao unao, umewahi kusomea au ni ujanja wako tu?

Kenny Guitar: Hapana sijasomea, ni ujanja tu na kujifunza mwenyewe YouTube.

BINGWA: Mpaka sasa umepata mafanikio yoyote kutokana na sanaa yako?

Kenny Guitar: Mafanikio ni mengi kama hivi kujulikana, nimeanza kupata hela ambazo nilikuwa sitarajii, kujuana na watu, nilikuwa nyuma ya migongo ya watu lakini sasa hivi nasimama mimi kama mimi.

BINGWA: Malengo yako ni yapi?

Kenny Guitar: Mimi nawaza kutoka nje kupiga gitaa, Marekani mbali hapo tu Nigeria, nataka siku moja Davido aniite nimpigie gitaa au hata Coke Studio tu hapo.

BINGWA: Changamoto gani unakutana nazo?

Kenny Guitar: Unakuta msanii unampigia gitaa prodyuza analiminya na kuweka vinanda vyake juu ili gitaa lisisikike, pia wengi kutoniamini kama naweza kufanya.

BINGWA: Una jambo gani la mwisho kwa mashabiki wa muziki?

Kenny Guitar: Kikubwa ni sapoti watu waje Instagram natumia @kennyguitar wanipe ushauri pia kwa sasa sina meneja na sihitaji kwa sasa kwa sababu nafikiri kutembea mwenyewe kwanza kwa miguu yangu mpaka hapo baadaye.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*