Katwila: Simba jiandaeni tunakuja

ZAITUNI KIBWANA

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila, ametoa mkwara mzito kwa wapinzani wao Simba kuwa wasitarajie mteremko watakapovaana nao keshokutwa.

Simba itawakaribisha Mtibwa Sugar Alhamisi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Akizungumza na BINGWA jana wakati akirejea kutoka mkoani Tanga, Katwila alisema licha ya mechi kuwa karibu karibu lakini Simba wasitarajie mteremko.

“Hakuna kupumzika mechi zipo karibu karibu sana, mfano hapa tunarudi kutoka Tanga tunapumzika kesho na keshokutwa tunaanza safari ya Dar es Salaam.

Alisema watakuwa na umakini mkubwa kupata matokeo kwenye mchezo huo na kuendelea kujiweka pazuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Tunapaswa kutumia nguvu kubwa, Simba si timu ya kubeza, hivyo tutapambana kufa au kupona kuhakikisha tunaibuka na ushindi,” alisema.

Mtibwa Sugar kwa sasa wapo nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara wakikusanya alama 49, katika mechi 35 walizocheza mpaka sasa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*