‘Kasi ya utafunaji fedha Yanga kubwa’

NA HUSSEIN OMAR

ALIYEKUWA mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Yanga, Tobias Lingalangala, amesema maisha ya dhiki wanayoishi wachezaji wa timu hiyo ya kutolipwa mishahara kwa wakati pamoja na stahiki zao nyingine, yamemfanya aachie ngazi klabuni hapo.

Lingalangala ambaye alishinda kwa kura nyingi katika uchaguzi uliopita, ni miongoni mwa viongozi bora waliowahi kutokea ndani ya klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Kigogo huyo amewahi kuwa Kaimu Mwenyekiti, licha ya sasa nafasi hiyo kushikiliwa Lukumay Samwel.

Alisema ni ngumu kuishi katika familia ambayo baba anakula vizuri na kulala pazuri, huku watoto wake wakiomba misaada kwa majirani pasipo kufahamu kesho yao itakuwaje.

Akizungumza na BINGWA jana, Lingalangala, alisema kasi ya utafunaji wa fedha ni kubwa kiasi cha kuwavunja nguvu matajiri ambao wamekuwa wakitamani kuwekeza fedha kwa vigogo hao wa soka hapa nchini.

Alisema klabu imekosa mvuto kwa matajiri wanaotaka kuwekeza kutokana na aina ya viongozi waliopo, ndio maana hata uchaguzi hawataki kufanya kwa sababu wengi wao hawana uhakika wa kurudi.

 “Unajua kupiga haikatazwi lakini ifike sehemu tuone huruma na hawa watoto sasa, binafsi nimeona nijitoe katika dhambi hii kubwa yasije kuja kunikuta makubwa,” alisema.

Alieleza katika kipindi chake cha uongozi, mara kadhaa aliwashawishi wenzake jinsi kiongozi bora anavyotakiwa awe, lakini alijikuta akifeli na kutengwa.

“Mambo ni magumu ndani ya Yanga kutokana na viongozi waliobaki kukosa huruma na wachezaji, ambao kula yao na mishahara imekuwa shida kuipata.

“Naipenda sana Yanga lakini kwa hapa ilipofika inatosha, kuna mambo mazito yanafanywa ambayo siwezi kuyataja humu kiufupi wenzangu hawana huruma na watoto hawa,” alisema Lingalangala.

BINGWA lilimtafuta Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samuel Lukumay, kuzungumzia juu ya kujiuzulu kwa mjumbe huyo na sababu zake ambapo alisema bado hawajapokea barua yoyote inayoonyesha kuachia kwake ngazi.

“Sisi hatujapata barua yoyote kutoka kwake na hizo sababu za fedha kutafunwa na viongozi, mwambie yeye akuthibitishie au akuonyeshe sawa, wewe uliongea naye wapi,” aliuliza Lukumay kabla ya kukata simu yake.

BINGWA halikuishia hapo, lilimtafuta pia Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Omary Kaya, kuzungumzia juu ya kauli hiyo na simu yale iliita bila kupokelewa.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*