Kama unaishangaa Serengeti Boys huwezi kuzipongeza Simba, Stars


NA HASSAN DAUDI

USHINDI wa mechi mbili tu ungetosha kuipeleka Tanzania katika fainali za Kombe la Dunia za vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwaka huu nchini Brazil.

Kuiweka vizuri, ndani ya mwaka mmoja, historia tatu zingekuwa zimeandikwa kwani tayari Simba na Stars zilishachukua nafasi. Wekundu wa Msimbazi walitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1994.

Stars nayo ilikata tiketi ya kushiriki fainali za Afcon za mwaka huu kule Misri. Kabla ya hilo kutimia mwezi uliopita, mashabiki wa kandanda nchini waliishia kuitazama michuano hiyo kupitia runinga tangu mwaka 1980.

Serengeti ilishindwa kuungana na Simba na Stars kuendeleza ndoto ya wadau wa kandanda la Tanzania, baada ya kupoteza mechi zote tatu za Kundi A la fainali za Afcon kwa vijana wenye umri huo, michuano ambayo ndiyo inayotoa nafasi nne za kwenda Brazil.

Huku hilo likishindikana, binafsi ningependa kuibuka na hoja tofauti kidogo ambayo msingi wake ni shutuma alizoelekezewa kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo, wakati michuano hiyo ya wiki mbili ikiendelea katika viwanja vya Taifa na Chamazi jijini Dar es Salaam.

Nikiri kuwa huenda kocha Mirambo ameponzwa na saikolojia ya mashabiki wa vijana wake. Isingekuwa rahisi kuwaaminisha Watanzania kuwa wanaikosa nafasi ya kwenda Kombe la Dunia kwa kukosa ushindi wa mechi mbili tu.

Kwa namna morali ilivyokuwa juu kabla ya mashindano, Mirambo na wasaidizi wake wa benchi la ufundi wanapaswa kukubali tu kwamba saikolojia ya wengi ilishatangulia Brazil, wakiamini hakuna cha kuizuia kwa kuwa ilikuwa katika ardhi ya nyumbani.

Kama ilivyo kwa mashabiki wote duniani, ingehitaji kazi kubwa kuwaaminisha Serengeti Boys haitakwenda na imeyaaga mashindano ya Afcon U-17, ikiwa imefungwa jumla ya mabao 12 katika mechi tatu dhidi ya Nigeria, Uganda na Angola.

Nikirejea katika hoja yangu, nianze kwa kutokubaliana na madai ya uenyeji kuwa ilikuwa sababu ya msingi kwa Serengeti Boys kuipeleka Tanzania. Licha ya kwamba ni dhana iliyozoeleka, soka la kisasa haliipi nafasi kubwa mbele ya ubora wa timu husika.

Bahati mbaya, hata historia ya michuano yenyewe haioneshi kuwa Serengeti Boys ilikuwa na nafasi ya ubingwa kwa kuwa ilikuwa nyumbani. Tangu mwaka 1995, ni Gambia pekee iliyoweza kuziandaa na kutwaa ubingwa wa fainali hizo. Pia, mwaka jana zilifanyika Gabon lakini Mali ndiyo iliyoibuka kidedea.

Katika kile nilichokiona, hakuna namna ya kuepuka ukweli kwamba kuvurunda kwa Serengeti Boys ni sehemu ndogo tu ya udhaifu mkubwa wa soka la vijana nchini, hivyo kuibua hofu juu ya njia iliyotumika kuzivusha Simba na Stars.

Wataalamu wa soka wanaweza kukubaliana na hoja yangu kwamba, ili kujijengea misingi imara katika ramani ya mchezo huo ulimwenguni, mafanikio ya timu ya taifa yanatakiwa kuakisiwa na hatua za chini (timu za vijana).

Nikizitolea mfano Hispania, mafanikio ya timu yao ya taifa yanaakisiwa na kile kinachofanywa na vijana wao wa chini ya umri wa miaka 17 ambao mwaka juzi walifika fainali ya Kombe la Dunia. Iko hivyo England, Ujerumani, Brazil na katika mataifa mengine yanayosifika kwa maendeleo ya kandanda.

Ingekuwa hivyo kwa Tanzania, basi timu nyingine saba zilizocheza Afcon U-17 pale Taifa na Chamazi zingeihofia Serengeti Boys hata kabla ya kutua nchini, zikitambua kuwa inatokea iliko Simba na Stars zilizotikisa Afrika mwaka huu.

Zaidi ya hapo, ni bahati na ujanjaujanja tu.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*