Kama mpenzi wako ana sifa hizi, amani kwako ni lazima

ANAKWAMBIA nakupenda huku anamaanisha. Ukimwangalia sura yake ni kama nayo inasema hivyo, midomo yake inaashiria anachosema hata macho yake ni kama yanamsapoti kwa kile unachokisikia kutoka kwake.

Kwake wewe si mtumwa, thamani yako kwake hata wewe mwenyewe unaiona. Hata ukipata matatizo unauhisi upendo wake.

Ni lazima awe karibu yako kukufariji, kukupa nguvu na kuhakikisha unarudisha uchangamfu na tabasamu lako ambalo huenda litakuwa limepotea.

Kukoseana ni tabia ya binadamu. Ikitokea hajifanyi ndiye Pilato wa kutoa hukumu tu- hapana. Ataangalia kosa na kutaka kujua ni kwa namna gani limetokea.

Msamaha si kitu kigumu kwake ikiwa utauomba kwa dhati na kuonesha kujutia ulilofanya. Suala la kuoana, kwenu haliwezi kuwa hadithi ya kufikirika.

Baada ya kila mmoja kuonesha kuridhika na mwenzake kuanzia mwonekano mpaka tabia. Taratibu za kuanza kuingia katika maisha ya mahusiano matakatifu itaanza.

Mdomo wake hauwezi kuwa kero kwako kwa maneno ya karaha na maudhi bali utakuwa ni faraja kwa maneno matamu na masihara.

 Anajua kwako yeye ndiyo chanzo cha furaha, katu hawezi kuruhusu kuona ukiumia ama ukalia kwa sababu yake. Labda kwa sababu njema za kimapenzi.

Kwakuwa kaamua kuwa na wewe basi hata ndugu zako pia anaona kama wake. Shida ikiwa kwenu anaona iko kwao. Kwako ni mshauri mwema kuhakikisha mnapambana na hali ya maisha.

Si mpayukaji hovyo.  Aibu yako ni aibu yake, ukifanya kosa haliwezi kuwa matangazo kwa wengine bali atahitaji mlimalize wawili ikiwa mnauwezo huo.

Hawezi kuwa nyuma kukuona ukipotoka wakati yeye yupo. Kila siku anajua hatua yako moja inamaana pia katika maisha yake. Hawezi kuruhusu kuona ukipotea.

Akiwa na wewe atahitaji kuona ukifurahia kila sekunde ya uwepo wake kwa sababu anajua ana dhima hiyo.

Daima hawezi kupenda kuona akikukosea. Ikitokea basi kamwe hawezi kuwa mvivu kuhitaji msamaha wako.

Akiulizwa umeolewa hajishauri kujibu. Kwa sababu mbali na wewe haoni mwingine wa kufaa kuwa na yeye.

Hawezi kuwa sawa na wale ambao wakiulizwa kama wameolewa wanasema hawapendi kuzungumzia habari hizo, lengo likiwa ni kukwepa kusema  wameolewa kwa sabau watakimbiza ‘bahati’ za kuwa na mahawara.

Hawezi kuwa na amani ukiwa na matatizo, ukiumwa ni kama na yeye anaumwa vile. Hawezi kukuacha ndani hoi kisha akaenda kufurahi na marafiki zake. Hawezi kuthubutu.

Ni mara chache sana kumwambia neno moja mara mbili. Yeye ni mwepesi sana kukuelewa. Anaheshima sana na wewe, hawezi kuwa kama wale anakuacha unaongea wee! Huku yeye akicheza ‘game’ kwenye simu. Siyo adabu.

Hawezi kukufanya kama kifaa, anajua wewe ni binaadamu. Ukisema umechoka si wa kukupiga vibao eti umpe- hapana.

Kwako daima ni mwelewa. Hata ukiwa mbali na yeye anaishi kama vile unamwona. Si ukiwa mbali basi ndiyo awe kama amefunguliwa vile- hapana.

Kama alikuwa anavaa hijabu basi atavaa, kama alikuwa haendi disko basi atakaa ndani tu. Haijalishi umbali uliopo, hata uwe Ulaya heshima yako itakuwa vile vile kwake.

Mapenzi yake kwako hayawezi kupanda ama kushuka kutokana na kipato chako. Yeye anaona ni vyema kama kupanda basi yapande kipindi ambacho hauna kitu si kile ambacho umeongezewa mshahara.

Ni mshauri mwema kwako. Si wa kila siku kutaka kununuliwa vito vya gharama tu, hapana. Anakumbuka na mambo ya maana yenye faida katika maisha yenu. Ni mnyenyekevu na mwenye subira.

Halazimishi wala hanuni bila sababu ya kueleweka. Mapenzi ni faraja na amani, katu hawezi kuruhusu ukose vitu hivi kwake. Kwako daima atakuwa mpiganiaji wa kila chenye kukufanya upate raha na starehe.ramadhanimasenga@yahoo.com


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*