Julio aipigia hesabu Transit Camp

NA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

KOCHA Mkuu wa Dodoma FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema timu yake imejipanga kuvuna pointi tatu katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) dhidi ya Transit Camp.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa keshokutwa katika Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam.

Dodoma FC inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Kundi B baada ya kujikusanyia pointi 15, huku vinara Boma FC wakiwa na pointi 18 wakifuatiwa na Arusha United pointi 17 sawa na Geita Gold.

Akizungumza na BINGWA jana, Julio, alisema mchezo huo ni muhimu kwao hivyo wamejipanga kuondoka na ushindi ili kujiwekea mazingira mazuri ya kupanda Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Alisema katika kikosi chao kulikuwa na  majeruhi wawili, Shabani Kisiga na Anwary Jabiri, lakini sasa wanaendelea vizuri hivyo atawatumia katika mchezo huo.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Fortunatus John ‘Foti’, alisema timu inatarajia kuondoka leo kuelekea jijini Dar es Salaam kuanza maandalizi ya mtanange huo.

“Kikosi kinaondoka kesho (leo) na Ijumaa tutafanya mazoezi katika Uwanja wa Azam Complex, uongozi unaendelea kupambana kuhakikisha wachezaji wanapata huduma zote muhimu, hivyo wasituangushe,” alisema Foti.


Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

*
*